******************************************
Hospitali ya Aga Khan kushirikiana na wadau mbalimbali wameungana kwa pamoja na kuandaa program ya awamu ya 5 itakayohusika na huduma ya upasuaji kwa wakina mama na watoto wakike masikini na walemavu kubadili na kuboresha maumbile au ngozi iliyokakamaa.
Programu hiyo itafanyika katika hospitali hiyo mnamo Juni 15 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana huku huduma hiyo ikiratibiwa kwa wakati mmoja kupitia vituo vya afya vya Aga Khani katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa, Mwanza, Tabora, Bukoba, Tanga na Bunda.
Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa Upasuaji kutoka hospitali ya Aga Khani Dkt. Aidan Njau amesema kuwa Wanawake na watoto wa kike maskini wenye ulemavu uliosababishwa na ukatili wa majumbani, kuungua moto na ajali wapatao 50 wanatarajiwa kunufaika na huduma ya upasuaji wa kubadili na kuboresha maumbile, ngozi iliyokakamaa ili kuwapa frusa ya kujiamini na kufanya shughuli za kiuchumi ndani ya jamii.
“Kwa kuwa upasuaji wa kuboresha maumbile, ngozi iliyokakamaa, umeonesha kuboresha kwa kiwango kikubwa maisha ya wale wanaosumbuliwa na unyanyapaa na ulemavu Hospitali ya Aga khan na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinayofuraha kushirikiana kwa mara nyingine tena katika mradi huu wa kipekee” Amesema Dkt. Njau.
Aidha ameongeza kuwa kwa sasa wanawake wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na Ugonjwa wa Saratani ambao umekuwa ukisababisha kuondolewa kwa titi lililoathirika hivyo watawafanyia pia upasuaji wa kuwawekea titi kupitia nyama zao ili kuwa na muonekano sawa na kuepuka kunyanyapaliwa ndani ya jamii.
Kwa upande wake Daktari Mkuu wa huduma za upasuaji kutoka Aga Khani Dkt. Arthar Ali amesema kuwa kutokana na uhitaji wa Upasuaji huo kuwa mkubwa wameamua kuhusisha nchi nzima na utafanyika kwa awamu mbili mwaka huu ukihusisha mikoa ya Dodoma, Morogoro, Mbeya, Iringa, Mwanza, Tabora, Bukoba, Tanga, Bunda ambako maeneo yote hayo yanavituo vya Afya vya Aga Khani hivyo wanawake na watoto wa kike kufika kwa ajili ya tathimini ya awali ya kuonwa na wataalamu.
Naye mmoja wa wawakilishi kwa wadau ambao wamewezesha zoezi hilo ambaye pia ni mwanzilishi wa SADAKA Network Dkt. Ibrahim Msengi amesema kuwa tatizo la ulemavu unaotokana na ukatili majumbani, kuungua moto na ajali bado ni kubwa ndani ya jamii hivyo wadau mbalimbali, Serikali na Sekta Binafsi washirikiane kwa pamoja katika kuwasaidia Wanawake na watoto wa kike maskini wanaonyanyapaliwa ndani ya jamii.