Mkuu wa kitengo cha wateja Binafsi NMB – Omari Mtiga (katikati) akimsikiliza Meneja mwandamizi wa wateja wa amana, Isaac Mgwassa (kulia) wakati wa ufunguzi wa hati fungani za benki hiyo jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Ushauri NMB, Sigifrida Joseph
Meneja Mwandamizi wa Ushauri NMB, Sigifrida Joseph, akizungumza wakati ufunguzi wa hati fungani za benki hiyo jijini Dar es Salaam jana. katikati ni Mkuu wa kitengo cha wateja Binafsi wa NMB – Omari Mtiga na kushoto ni Meneja Mwandamizi wa wateja wa amana NMB Isaac Mgwassa
************************************************
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB, imeanza mauzo ya Hati Fungani ‘NMB Bond’ yenye riba ya asilimia 10 kwa wateja na wasio wateja wa benki hiyo waliopanga kuwekeza fedha zao ili kupata faida nzuri kwa kipindi cha miaka mitatu, kima cha chini kikiwa ni Sh. 500,000.
Akizungumza Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Omari Mtiga, alisema hii ni mara ya pili kwa NMB kutoa Hati Fungani ya aina hiyo, inayoweza kununuliwa kupitia matawi na mawakala wao kote nchini.
“Kufunguliwa kwa Hati Fungani ya NMB ni matokeo ya ruhusa kutoka kwa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana Tanzania (CMSA), ambako mwekezaji wa Hati Fungani watapata riba ya asilimia 10 kwa mwaka itakayolipwa kila miezi mitatu kwa miaka yote mitatu,” alisema Mtiga.
Aliongeza ya kwamba, Hati Fungani zitauzwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia jana Juni 10 hadi Julai 8 mwaka huu, ambapo miaka mitatu ya hati hizo itafikia ukomo Juni 2022. Mara ya mwisho NMB kutoa Hati Fungani ilikuwa ni Juni 17, 2016.
“Kupitia Hati Fungani hizi, NMB inatarajia kutunisha mfuko kwa kiasi cha Sh. Bilioni 25, huku tukiwa na ruhusa ya kuongeza hadi kufikia Sh. Bilioni 40, kama ilivyotokea mara ya mwisho tulipotoa Hati Fungani hizi mwaka 2016.
“Kutokana matokeo chanya ya Hati Fungani iliyopita, wawekezaji wengi wameonyesha nia ya kuwekeza, nasi tunaitumia hii kama fursa muhimu katika kukidhi kiu yao, jambo litakalochangamsha uendelezaji wa masoko ya mitaji nchini,” alisisitiza Mtiga.
Aidha, alifafanua ya kwamba, bada ya mwezi mmoja wa mauzo kufungwa, Hati Fungani ya NMB inaweza kupatikana kwa mteja mmoja kumuuzia mwingine, hivyo kupata fedha kabla ya kukomaa (yaani kipindi cha miaka mitatu), fursa inayomuwezesha mteja kuongeza Hati Fungani yake.
Mtiga alibainisha kuwa, ili kununua Hati Fungani ya NMB, mteja anatakiwa kutembelea tawi lolote miongoni mwa matawi 229 ya NMB nchini kote, au kulipia kwa mawakala na kisha kwenda matawini kufanya usajili rasmi.