Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto)
akizungumza na Viongozi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama
(Polisi, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji) vinavyofanya kazi katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakati
alipofanya ziara ya kuvikagua vyombo vyake vitakavyotoa
huduma uwanjani katika uwanja mpya wa Terminal III
unaotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni. (Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimuuliza
swali Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege, Paulo Rwegasha
(watatu kushoto), wakati alipofanya ziara katika Uwanja wa Ndege
cha Julius Nyerere (JNIA-Termila III) kwa ajili ya kuvikagua
vyombo vyake vitakavyotoa huduma katika Uwanja huo
unaotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni. (Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja
Jenerali Jacob Kingu, akizungumza katika kikao kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola,
(wapili kulia), kuzungumza na maafisa wa Jeshi la Polisi, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara ya Uhamiaji ambao watatoa
huduma katika Uwanja mpya wa Ndege wa Julius Nyerere
Terminal III unaotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni. (Picha na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala,
akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi
Lugola (kushoto), na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali
Jacob Kingu, katika moja ya ofisi zitakazotumiwa na Maafisa wa
Uhamiaji kwa ajili ya ukaguzi wa wasafiri watakaotumia Uwanja
mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, unaotarajiwa
kutumika hivi karibuni. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini
(TAA), Injinia Julius Ndyamukama akimfafanulia jambo Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, (wapili kushoto),
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu (watatu
kushoto), na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ramadhan
kailima (kushoto), wakati Waziri huyo alipofanya ziara Uwanja
mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili
ya kuvikagua vyombo vyake ambayo ni Jeshi la Polisi, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji vinavyotarajiwa kutoa
huduma hivi karibuni. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi)
Msimamizi wa Mradi kutoka Wakala wa Ujenzi (Tanroad) Burton
Komba akimwelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi
Lugola, (aliyeshika kitabu), sehemu mbalimbali za Uwanja mpya
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati Waziri huyo
alipofanya ziara ya kuvikagua vyombo vyake ambayo ni Jeshi la
Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Uhamiaji vinavyotarajiwa kutoa huduma hivi karibuni. Wapili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu, na kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
**********************************
Na Felix Mwagara
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal III) ya kuvikagua vyombo vyake vinavyotarajiwa kutoa huduma katika uwanja huo hivi karibuni.
Waziri Lugola aliwasili katika uwanja huo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake, pamoja na taasisi zake, ambapo walipokelewa
na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA).
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi uwanjani hapo, Waziri Lugola alisema hana shaka na utoaji wa huduma wa vyombo vyake katika uwanja huo mpya, kwa kuwa ameridhika na mipango ya utoaji huduma wenye weledi baada ya uwanja huo kufunguliwa.
“Wizara yangu ni wadau wakubwa katika utoaji huduma katika uwanja huu wa
ndege, ni lazima nijue Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Idara ya Uhamiaji, wamejipangaje katika kutoa huduma bora kabisa hapa uwanjani, sina shaka nao nimeridhika baada ya kumaliza ukaguzi,” alisema Lugola.
Pia Waziri Lugola, alimuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Injinia Julius
Ndyamukama, kuwa ameridhishwa na mpangokazi wa vikosi hivyo kwa namna
viulivyojipanga kutoa huduma katika uwanja huo mpya.
“Nimeridhishwa na utendaji kazi wa Vyombo vya ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara yangu kwa namna vilivyojipanga juu ya utendaji kazi na jinsi watakavyotoa huduma kwa wasafiri wa uwanja huu, ila nimepewa baadhi ya changamoto chache na tunaahidi kuzifanyia kazi mapema kabla ya uwanja huu kufunguliwa,” alisema Lugola.
Lugola alihakikishiwa na viongozi wa majeshi hayo kuwa, watafanya kazi kwa nguvu zote kwa kutoa huduma bora katika uwanja huo.
“Tupo tayari kuutumikia umma na kwa kuwa kazi zetu ni kuusaidia umma wa
watanzania tupo tayari kuhakikisha uwanja huu mpya pamoja na viwanja vyote
vinakuwa salama muda wote.” Alisema Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Anna
Makakala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Injinia Julius Ndyamukama,
alimshukuru Waziri huyo pamoja na viongozi wa Wizara kwa kufika uwanjani hapo kufanya ukaguzi, ila alimuomba waziri huyo magari ya zimamoto yaongezwe ili kuhudumia uwanja huo mpya.