Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto katika Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya
moyo kwa watoto Dkt. Naiz Majani akisimamia upimwaji wa mtoto ndani ya
jengo la Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto cha taasisi hiyo
ambalo lilitolewa mwaka jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Jengo hilo ambalo
limemalizika kukarabatiwa mwezi uliopita na tayari limeshaanza
kupokea wagonjwa, lina vitanda 40 kwa ajili ya watoto tu, na pia lina
vitanda 8 kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watoto tu na muda
wowote kuanzia sasa litafunguliwa rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo Prof. Mohammed Janabi akiwa na Mkuu
wa Kitengo cha Matibabu ya Moyo kwa Watoto katika taasisi hiyo ambaye
pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa taasisi hiyo
Dkt. Naiz Majani wakibadilishana mawazo nje ya jengo la Kitengo cha
Matibabu ya Moyo kwa Watoto cha taasisi hiyo ambalo lilitolewa mwaka
jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli. Jengo hilo ambalo limemalizika kukarabatiwa mwezi uliopita
na tayari limeshaanza kupokea wagonjwa, lina vitanda 40 kwa ajili ya
watoto tu, na pia lina vitanda 8 kwa ajili ya wagonjwa mahututi (ICU)
kwa watoto tu na muda wowote kuanzia sasa litafunguliwa rasmi
*****************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo Prof. Mohammed Janabi amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kwa kuisaidia Taasisi hiyo kupata jengo la Kitengo cha Matibabu ya
Moyo kwa Watoto.
Prof. Janabi amesema mwisho mwa wiki kwamba kufuatia maelekezo ya
Mhe. Rais Magufuli aliyoyatoa mapema mwaka jana (2018), moja ya
majengo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili lililopo jirani na Taasisi
hiyo lilikabidhiwa kwa Taasisi hiyo na Serikali ikatoa fedha za
kulikarabati na kuwekewa miundombinu ya kutolea huduma za matibabu ya
moyo kwa watoto.
Ameongeza kuwa jengo hilo lina lina vitanda 40 vya kawaida na vitanda
8 vya watoto wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na kwamba kukamilika
kwake kutaiwezesha Taasisi hiyo kupata vyumba vipya 4 vya kliniki
ambavyo vitawawezesha Madaktari kuwaona watoto 60 kwa siku.
Prof. Janabi amebainisha kuwa kabla ya kupatiwa jengo hilo, Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete ililazimika kuwachanganya watoto na watu wazima
katika sehemu moja iliyojumuisha chumba cha ICU, wodi na pia kliniki
ambayo iliwawezesha Madaktari kuona wagonjwa kati ya 25 na 30 tu kwa
siku.
“Kwa furaha kubwa kabisa, mwezi uliopita jengo letu limekwisha kama
unavyoliona lina vitanda 40 kwa ajili ya watoto tu, lina vitanda 8 kwa
ajili ya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watoto tu na muda wowote kuanzia
sasa tutalifungua.
“Sasa nini faida kubwa ambayo tutaipata sisi kama Madaktari, sasa hivi
watoto wagonjwa wakitoka chumba cha upasuaji (Theatre) watakwenda moja
kwa moja kwenye ICU ya watoto, hii ni tofauti na hali ilivyokuwa
kwenye hili jengo kubwa tulilokuwepo ambapo Daktari alikuwa anaingia
wodini anamuona mgonjwa wa kwanza mtu mzima ana kilo 90, kitanda
kinachofuatia kuna mtoto ana kilo 5 ambaye pia tumemfanyia upasuaji,
kwa hiyo uwezekano wa kufanya makosa ulikuwa mkubwa sana iwe kwenye
kutoa dawa au huduma nyingine. Ndio maana tunamshukuru sana Mhe. Rais
Magufuli kwa kutusaidia na ufanisi wetu wa kazi utakuwa mkubwa zaidi”
amesema Prof. Janabi.
Aidha, Prof. Janabi amewashukuru wadau binafsi waliochangia ukarabati
wa jengo hilo wakiwemo Jumuiya ya Kihindi ya BAPS na Benki ya CRDB
waliofanikisha kukamilika kwa jengo hilo.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa
taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani amesema tatizo la magonjwa ya moyo hapa
nchini ni kubwa ambapo katika kila watoto 100 wanaozaliwa 1 ana tatizo
la moyo hivyo kujengwa kwa jengo hilo kuna umuhimu mkubwa kwa
Watanzania ambao awali walikosa huduma ama kulazimika kwenda nje ya
nchi.