*****************************
MEYA Mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda amesheherekea sikukuu ya Eid-El Fitr kwa kujumuika na watoto yatima wanaoelelea katika kituo cha Maunga, kilichopo Hananasif Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam
Mwenda aliungana na watoto hao kwa kujumuika katika chakula cha mchana alichokuwa amekiandaa yeye na familia yake nyumbani kwake eneo la Mikocheni na kuwataka watoto hao kutia mkazo katika masomo ili waweze kuja kulitumikia Taifa hapo baadae.
Akizungumza na watoto hao, Mwenda aliwataka kutojiona kama wametengwa na kwamba jamii ipo pamoja nao wakati wote hivyo suala la msingi kwao ni kuendelea kuwa watoto wema kwa kumcha Mungu wakati wote bila kusahau kuwaombea dua wale wote wanaowalea na kuwakumbukuka kwa namna mbalimbali.
“Tieni mkazo katika masomo yenu wakati wote mnapokuwa shuleni na hata nyumbani, kumbukeni kuwa elimu ndio urithi wenu mkubwa zaidi ya kitu kingine chochote, mkumbuke pia kusali na kuwaombea njema kwa Mungu wale wote wanaowakumbuka” alisema Mwenda.
Kwa upande wao watoto hao, walimshukuru Mwenda kwa hatua yake ya kuwa pamoja nao siku hiyo na kumtaka kuendelea kufanya hivyo wakati mwingine anapojaliwa uwezo.
Walisema kitendo cha Mwenda kujumuika nao amekuwa akikifanya kila mwaka huku wakiwaomba watu wengine wenye uwezo kuiga kitendo cha Meya huyo mstaafu kwani kinawafanya wasijikie faraja na kujiona kama watoto wengine wanaolelewa na wazazi wao.
Mbali na vyakula na burudani mbalimbali yakiwemo mashindano ya kuimba kucheza, watoto hao pia walizawadiwa zawadi mbalimbali yakiwemo madaftari, mabegi ya shule jambo lililowafanya watoto hao kufurahia.