Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard akitoa mada kuhusu Mkaa endelevu kwa maofisa mbalimbali kutoka wilaya 19 nchini.
Meneja Mradi was Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) maarufu Mkaa Endelevu Charles Leonard akitoa mada kwa maofisa mbalimbali kutika Serikali za Mitaa.Picha na Suleiman Msuya.
*****************
NA SULEIMAN MSUYA
MRADI wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) maarufu ‘mkaa endelevu’ umenikiwa kuingizia halmashauri, vijiji na wananchi zaidi ya shilingi bilioni 3 kuanzia 2014 hadi sasa.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa TTCS, Leonard Charles wakati akiwasilisha mada kwa maofisa mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Serikali Kuu walikutana mkoani Morogoro.
Meneja alisema mradi wa TTCS unatekelezwa katika vijiji 30 vya wilaya za Mvomero, Kilosa na Morogoro chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Mtandao wa Jamii wa Kusimamia Misitu Tanzania (Mjukita), Shirika la Kuendeleza Nishati Asili Tanzania (TaTEDO) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC).
Alisema katika mradi huo vijiji 22 vimeanza kunufaika katika pande mbili ambazo ni kiuchumi na utunzaji wa mazingira huku nane vikiwa katika mchakato.
Alisema hadi kufikia mwezi Mei 2019 vijiji vimeweza kikusanya mapato halali zaidi ya shilingi bilioni 1.4, wachomaji mkàa shilingi bilioni 1.2 na halmashauri shilingi milioni 500.
Meneja alitaja baadhi ya vijiji ambavyo vimenufaika na mradi ni Ulaya Mbuyuni, Matuli, Kitunduweta, Mlilingwa, Ulaya Kibaoni, Diguzi na vingine.
Leonard alisema mradi wa mkaa endelevu ulianza Machi 2012 katika vijiji 10 lakini baada ya kuonekana mafanikio wamelazimika kuongeza vijiji hadi kufika 30.
“Mradi wa TTCS maarufu mkaa endelevu umefanya mapinduzi makubwa kiuchumi, kijamii na maendeleo katika vijiji vilivyopo kwenye mradi kama kuboresha sekta ya afya, elimu, maji, kilimo na mitaji,” alisema.
Alisema mafanikio ya mradi yamezingatia kutoa elimu kwa jamii husika, watendaji na wafanya maamuzi hivyo kurahisisha utekelezaji.
Meneja alisema pia utekelezaji unazingatia uwepo wa mpango wa matumizi bora ya ardhi za vijiji, kutenga maeneo madogo ya mradi na kuvuna kwa kutumia vitalu.
Alisema pia mradi umefanikisha ujenzi wa ofisi za vijiji hali ambayo inarahisisha usimamizi wa mradi.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TFCG, Bettie Luwuge alisema warsha hiyo ya siku tatu imelenga kujenga uelewa kwa pande zote ili kurahisisha utunzaji wa misitu nchini.
Luwuge alisema rasilimali misitu ikitunzwa kwa ushirikiano wa wadau wote inaweza kubadilisha jamii kiuchumi na maendeleo.
“Tumeamua kukutanisha maofisa kutoka sekta ya kilimo, misitu, maliasili na sheria wa wilaya 19 lengo ni kuweza kubadilishana mawazo namna ya kutunza misitu yetu ili iwe endelevu,” alisema.
Alitaja wilaya husika kwa warsha hiyo ni Kigoma, Kilwa, Tabora, Namtumbo, Handeni, Kilindi, Mvomero, Morogoro, Kilosa, Lindi, Liwale, Tunduma, Kilolo, Ruangwa, Nachingwea, Mpwapwa, Songea, Nyasa, Mbinga.
Awali akifungua warsha hiyo Ofisa Misitu wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa alisema warsha hiyo itasaidia kuongezea uelewa maofisa hao kuhusu utunzaji misitu ya vijiji.
Chuwa alisema rasilimali mali misitu ikitunzwa kwa dhana ya uendelezaji itasaidia jamii kuinuka kiuchumi.