Home Mchanganyiko MATAJIRI WASHAURIWA KUSAIDIA WASIOJIWEZA

MATAJIRI WASHAURIWA KUSAIDIA WASIOJIWEZA

0

MFANYABIASHARA wa Madini Zakaria Nzuki, akishiriki kula chakula na watoto yatima .Chakula hicho kiliandaliwa kwa ajili ya sikukuu ya Idd el Fitri na MFANYABIASHARA huyo kwa kushirikiana na BAKWATA Mkoa wa Mwanza.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke akizungumza kwenye hafla ya chakula kilichoandaliwa na BAKWATA ikishirikiana na MFANYABIASHARA Zakaria Nzuki kwa ajili ya watoto yatima.

********************************

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

JAMII ya watu wenye kipato na nguvu kubwa ya kiuchumi (matajiri) wametakiwa kutumia sehemu ya mapato yao kusaidia wenye mahitaji wasiojiweza,yatima na wajane.

Rai hiyo ilitolewa jana na mfanyabiashara wa madini, Zakaria Nzuki kwenye chakula alichokiandaa kwa ajili ya watoto yatima 296 wanaolelewa katika vituo vya Taqwa, Mabatini, Imamu Hapsh na misikiti tofauti tofauti jijini Mwanza.

Alisema kuwa kwenye sikukuu ya Idd el Fitri akishirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Mwanza aliandaa hafla ya kula chakula na watoto yatima ambao baadhi yao hawana wazazi baada ya kufariki,walemavu na waliotelekezwa.

Nzuki ambaye kiimani ni Mkristo alisema matajiri na watu wengine wenye uwezo mzuri wa uchumi (kipato) wanapaswa kuangalia jamii wanayoishi nayo na kusaidia watu wasiojiweza na binafsi anafanya hivyo kwa sababu riziki anayoipata Mungu huigawa kupitia kwa watu wengine.

“Sote ni binadamu tumeumbwa na Mungu ambaye anagawa riziki za watu (yatima,wajane na wenye umaskini mkubwa wa kipato).Wakati mwingine anagawa kupitia kwetu hivyo ni vizuri kutumia sehemu ya mapato yetu kuwakumbuka watu wa namna hiyo,”alisema.

Mfanyabiashara huyo wa madini alisema ni muhimu matajiri wenye uwezo kiuchumi kurejesha kwa Mungu sehemu ya mapato yao (sadaka na zaka) kupitia kwa jamii na  kusaidia watu wenye mahitaji, ingawa ni wito lakini waone na wasukumwe na utashi wa nafsi zao.

 “Jambo hili kulifanya linahitaji utashi na msukumo wa nafsi, hivyo tuliojaliwa uwezo kiuchumi tuwasaidie maskini wasiojiweza ili kutimiza matakwa ya Mwenyezi Mungu ya kusaidia yatima,wajane na wenye shida mbalimbali.Binafsi nitaendelea kufanya hivyo kadiri nitakavyojaaliwa na Mungu,” Nzuki.

Alidai ni mwaka wa pili kwake kuandaa chakula na kula pamoja na watoto yatima na anafanya hayo kupitia taasisi za dini ambazo zinafahamu changamoto za jamii na makundi ya wenye mahitaji kwa karibu na hivyo kuwa rahisi kuwapata wahitaji kwa urahisi na kuwasaidia kwa pamoja, kwa wakati mmoja.

Naye Kaimu Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hassan Kabeke alisema, kitendo cha Nzuki kuandaa chakula na kula na yatima pamoja anatapa thawabu kubwa kutoka kwa Allah (Mwenyezi Mungu) na kuwataka wengine kujifunza kutoa robo ya mapato yao kwa ajili ya jamii.

Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula ambaye pia alishiriki chakula hicho na watoto hao alisema BAKWATA imeshiriki masuala ya kijamii bila kubagua. jambo ambalo taasisi zingine zimeiga na kushindwa si kwa uwezo bali uhusiano na bila uhusiano ni ngumu kufanikiwa