*******************************************
Kufuatia soko la mahindi kuporomoka kwa zaidi ya miaka mitatu hapa nchini na kuwasababishia hasara kubwa wakulima , serikali mkoani Njombe imewataka wakulima kufanya kilimo chenye tija ili kuzalisha mazao yatakayo kuwa na uwezo wa kumudu ushindani katika soko la ndani na kimataifa .
Serikali imefikia hatua mara baada ya kupokea kilio cha soko kutoka kwa wakulima na kufanya utafiti ambao umebaini kuwa mazao mengi yamekuwa yakizalishwa kwa ubora mdogo na kusababisha wanunuzi wengi kushindwa kununua malighafi hiyo ambayo huozea gharani huku wengine wakilazimika kuuza kwa hasara.
Wakizungumza mara baada ya kuwakutanisha wanunuzi na wakulima wa zao la mahindi kutoka wilaya zote za mkoani Njombe kupitia mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani katika zao la mahindi afisa kilimo mkoa Wilson Joel na Deogratus Mtewele mkurugenzi msaidizi kutoka Mtewele General Traders wamesema wakulima wengi wamekuwa wakifanya kilimo cha mazoea hatua ambayo inasababisha kupata mazao yasio na ushindani sokoni na kuwataka kubadilika ili kuendana na soko la kimataifa.
Samson Gunda na Paul Peter ni baadhi ya wanunuzi wakubwa wa malighafi ya mahindi mkoani Njombe ambao wanaelezea changamoto ya ubora inavyokwamisha soko la zao hilo linalozalishwa kwa wingi mkoani humo na kusababisha kuozea gharani kwakukosa soko.
Kwa upande wa wakulima akiwemo Asia Kabelege na John Kapanga wanasema kukosekana kwa bei elekezi , upungufu wa watalaamu wa kilimo ni miongoni mwa sababu zinazosababisha wengi wao kupata hasara kwa kuwa kumekuwa na walanguzi ambao wanatumia nafasi ya kukosekana kwa soko la uhakika la mahindi kupita vijiji kununua kwa bei ndogo ambapo wanadaiwa kununua kg 20 kwa shilingi elfu 4 hadi elfu 5 na kuwasababishia kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.
Katika mkutano huo wakulima na wanunuzi kutoka wilaya ya Ludewa, wanging’ombe ,Makete na Njombe wamekutana kujadili Soko la mahindi ambalo limeporomoka tangu mwaka 2017 hadi sasa.