Watumishi wa Tanroads Mkoani Manyara, wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kupanda miti 100 pembeni ya barabara kuu ya Babati-Singida katika wiki ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Meneja wa Tanroads Mkoani Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa katikati (mwenye kofia) na watumishi wengine wa Tanroads wakishiriki kusafisha mazingira ya mjini Babati kwenye wiki ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Mkuu wa mipango wa Tanroads Mkoani Manyara, mhandisi Dutu Masele (kulia) na mhasibu Julieth Kyaruzi wakishiriki kupanda mti kati ya miti 100 iliyopandwa na watumishi wa Tanroads Manyara.
******************************************
ANROADS MANYARA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI
MENEJA wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) Mkoani Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa ameongoza wafanyakazi wa mkoa huo kwa kupanda miti 100 na kusafisha mazingira ya Mjini Babati katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani.
Mhandisi Rwesingisa ameongoza maadhimisho hayo ya siku ya mazingira dunia walioadhimisha kwa siku tano, kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza mjini Babati, mhandisi Rwesingisa alisema katika maadhimisho hayo kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Tanroads Manyara, wamefanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema wamefanya maandamano ya kufanya usafi, utoaji elimu kwa umma na kuotesha miti katika barabara kuu na za mkoa huo zinazomilikiwa na Tanroads mkoani humo.
Alisema wamesafisha alama za barabarani na kuondoa zilizoharibiwa na kurudisha alama za barabarani zilizoibiwa au kuharibiwa.
“Pia wafanyakazi wa Tanroads mkoani Manyara kwenye wiki ya maadhimisho hayo wamepanda miti 100 na mingine 100 inatarajiwa kupandwa pembeni ya barabara kwa lengo la utunzaji mazingira,” alisema mhandisi Rwesingisa.
Alisema pamoja na kuotesha miti na kufanya usafi wa mazingira katika hifadhi ya barabara pia wamezibua mitaro na kufyeka nyasi kandokando mwa barabara.
“Tumefanikisha pia kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari na vipeperushi kuhusu hifadhi ya barabara na utunzaji wa mazingira ya barabara kuu na ya mikoa,” alisema mhandisi Rwesingisa.
Mmoja kati ya wafanyakazi wa Tanroads mkoani Manyara, Julieth Kyaruzi alisema amefurahia kushiriki kwenye maadhimisho hayo akiwa na watumishi wenzake.
“Kwa hizi siku nne tumefanya kazi mbalimbali za mikono yetu kwa pamoja katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani kwa hapa hapa mkoani kwetu Manyara,” alisema Kyaruzi.