Mhe.Waitara akiangalia ubora wa matofali yanayotengenezwa na kikundi cha jikomboe kilichopo eneo la Dodoma Makulu jijini Dodoma. Kikundi hiki kilikopesha shilingi milioni 10 na jiji la Dodoma na tayari kimerejesha shilingi milioni 2.5
Ujenzi unaoendelea wa jengo la stendi ya Mabasi na Soko katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma. Majengo hayo yatakapokamilika yanatarajia kugharimu shilingi bilioni 34.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe. Mwita Waitara akizugumza na walimu na wanafunzi katika shule ya sekondari ya Wella iliyopo eneo la Mkonze katika jiji la Dodoma.
Mhe. Watara akisalimiana na Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wella Mwanafunzi Grace Kabuta jana wakati Mhe. Naibu Waziri alipotembelea shule hiyo.
……….
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Serikali imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha kuwa wanaelekeza fedha wanazozikusanya kutoka katika vyanzo vyao mbalimbali katika kuboresha miradi na miundombinu ya jamii ili kuchochea kasi ya maendeleo katika halmashauri zao.
Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Mhe. Mwita Waitara wakati akiwa katika shule ya sekondari ya Wella iliyopo eneo la Mkonze katika jiji la Dodoma.
Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri hawana budi kutumia vizuri mapatao inayoyakusanya kuboresha miradi ya maendeleo kwani serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutatua changamoto na kero mbalimbali kwa jamii.
“Napenda kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe kuwa wanayaelekeza fedha wanazokusanya katika kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili halmashauri zao badala ya kusubiri kero hizo zishughulikiwe na serikali kuu,” amesema.
Naibu Waziri ameongeza kuwa changamoto kama za ukosefu wa matundu ya kutosha ya vyoo, uchakavu wa miundo mbinu ya shule, na kero nyingine za aina hiyo zinaweza kutatuliwa kwa kupitia makusanyo ya halmashauri husika.
Mbali na kutembelea sekondari ya Wella, ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za majengo yake yote kutokamilika na upungufu wa matundu ya vyoo, Naibu Waziri pia alitembelea eneo la Dodoma Makulu ambapo alijionea namna kikundi cha vijana cha Jikomboe kinavyojishughulisha na ufyatuaji wa matofali, kikiwa ni miongoni mwa vikundi mbalimbali vilivyopata fedha za mkopo kutoka halmashauri ya jiji la Dodoma.
Pia Mhe Waitara ametembelea eneo la Ipagala na kuona ujenzi wa shule ya mfano unavyoendelea , mradi wa kimkakati wa ujenzi wa soko na stendi wenye thamani ya shilingi bilioni 34, sekondari ya miyuji kukagua umaliziaji wa vyumba sita vya madarasa, na sekondari ya msalato kukagua ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa jiji la Dodoma bwana Godwin Kunambi alimweleza Naibu Waziri juu ya mikakati ya jiji hilo katika kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili shuke za msingi na sekondari ambapo amesema kuwa katika bajeti ijayo jiji limetenga kiasi cha shilingi bilioni 8 kutatua changamoto hizo.
Amesema kuanzia sasa jiji la Dodoma litahakikisha kuwa ujenzi wa shule zake utakuwa wa kisasa unaoendana na taswira ya jiji la Dodoma ambapo chini kutawekwa marumaru badala ya sakafu kama ilivyo hivi sasa na juu bati zake zitawekwa rangi kulingana na mpangilio wa ujenzi wa jiji hilo.
Akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikabili shule ya sekondari ya wella ambayo majengo yake mengi hayajakamilika licha ya kuanza kutumiwa na walimu na wanafunzi wa shule hiyo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa kwa mwaka huu jiji lilipeleka shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa baadhi ya miundombinu ya shule na kwamba wanatarajia kuwa katika mwaka ujao wa fedha majengo yote ya shule hiyo yatakarabatiwa kwa kuwekewa marumaru na mabati kupakwa rangi pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo vya walimu na wanafunzi.
Katika ziara yake hiyo ambayo ni ya kwanza kutembelea jiji la Dodoma kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Mhe. Waitara aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mhe.Patrobas Katambi, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma bwana Godwin Kunambi na viongozi mbalimbali kutoka mkoa wa Dodoma na jiji la Dodoma