Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa hospitali wakimsikiliza mwenyekiti wa bodi, Prof. Majinge leo.
Mkurugenzi wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru akisisitiza jambo kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi leo
Wajumbe wakifuatilia mkutano leo.
Afisa Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi. Christine Temba akitoa mada kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Muhimbili
Baadhi ya wajumbe wakihesabu kura baada ya kupiga kura kumchagua katibu na katibu msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi la Muhimbili.
Wajumbe wakifuatilia shughuli ya kuhesabu kura leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Charles Majinge akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi leo.
***********************************
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wametakiwa kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo ili kufikia malengo ya utoaji wa huduma bora za ubingwa wa juu.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Prof. Charles Majinge wakati akizindua Baraza jipya la Wafanyakazi.
Baraza limeshauriwa pia kusimamia majengo, matumizi ya fedha, vitendea kazi pamoja na utendaji wa wafanyakazi ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora za afya.
“Heshima ya Muhimbili katika kutoa huduma bora za afya imerudi. Ni lazima tuifanye Muhimbili iwe Hospitali ya Taifa kwa maana tuendelee kutoa huduma bora za kibingwa, tuwe kimbilio la wagonjwa,” amesema Prof. Majinge.
Prof. Majinge amelitaka baraza kutunza Muhimbili yakiwamo majengo na vitendea kazi kwa ajili ya vizazi vijavyo na kwamba wafanyakazi wanatakiwa kuthamini sehemu ya kazi kwa kuwa ni mahali ambako wanatumia muda mwingi kazini kuliko majumbani.
Katika kikao, Prof. Majinge amewataka wajumbe kutatua changamoto zinazojitokeza sehemu ya kazi ikiwamo migogoro ili kuimarisha utendaji kazi.
Awali, wakati akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi kuzindua Baraza hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Lawrence Museru amewataka wajumbe wa Baraza kuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa kuhimizana kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Amesema ni muhimu kuhakikisha kila mjumbe wa Baraza hili anatumia nafasi aliyopewa kama kiongozi ili uwakilishi wake uweze kuleta tija mahali pa kazi