*********************
Msaada tutani
MEYA Mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni ameahidi kugharamia mafunzo kwa ajili ya walimu wa Madrassa zilizopo katika Wilaya ya Kinondoni kwa ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi walimu hao ili kuongeza tija katika kueneza dini hiyo.
Meya Mwenda alitoa ahadi hiyo wakati wa futari aliyoiandaa maalumu kwa ajili ya walimu hao, wakiwemo maustadhi na Masheikh wa Misikiti mbalimbali iliyopo katika wilaya hiyo akiitikia ombi la Sheikh wa Wilaya ya Kinondoni Mohammed Mhenga aliyemuomba kufadhili mafunzo hayo.
Katika futari hiyo aliyokuwa ameiandaa katika makazi yake Mikocheni Jijini Dar es Salaam, Mwenda alisema mafunzo kwa walimu hao ni jambo asiloweza kulipa ugumu kwa kuwa anatambua thamani yao na hasa katika uenezaji na uendelezaji wa dini hiyo.
“ Natambua kazi nzuri mnayoifanya katika kufundisha dini ya Uislam hasa kwa watoto wetu na jamii ya watu wengine, nimelipokea suala hili na nipo tayari kushirikiana nanyi wakati wowote mtakaponiambia kuwa mpo tayari” alisema Mwenda.
Aidha alisema kitendo chake na kuwaalika walimu hao na kufuturu nao pamoja, kimelenga kuwatambua na kuthamini mchango wao mkubwa wanaoutoa kuiendeleza Quran ambayo ilishushwa ndani ya mwezi wa Ramadhan maalumu kwa ajili ya waumini wa dini ya kiislam pamoja na waamini wengine.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya kuindeleza dini hii, kwa hakika mnabeba thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, naamini siku moja atawalipa kama siyo hapa duniani basi akhera” alisema Meya huyo Mstaafu.
Awali Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mohammed Mhenga mbali na kumpongeza Mwenda kwa hatua yake ya kufuturu na walimu hao, aliwataka walimu hao kuzidisha elimu wanayoitoa kwa vijana kwa lengo la kuzidi kuieneza dini hiyo.
Aidha alisema kumalizika kwa mwezi mtukufu kusiwafanya waislam kubadirika na kugeuka kutenda matendo yenye kumchukiza Mungu na badala yake waendelee kusimama kikamilifu na kumuabudu mwakati wote.