…………………..Na Mwandishi Wetu.WITO umetolewa kwa halmashauri zote nchini kununua hisa za Benki ya Biashara ya DCB kwani licha ya kupata faida bali pia kunufaika na namna benki hiyo ilivyo na uzoefu katika kushirikiana na Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam katika suala la uendeshaji wa mitaji ya kifedha na usimamizi bora wa fedha.Akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Josephat Kandege aliyasema haya wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 17 wa Mwaka wa Wanahisa wa DCB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.Alisema kwa nyakati tofauti ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikitoa maelekezo kwa halmshauri nyingine ziige mfano wa Manispaa ya Dar es Salaam kwa kununua hisa za Benki ya DCB ambayo kimsingi ndio chimbuko la kuanzishwa kwa benki hii.Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Kandege alitoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa DCB, menemejimenti na wafanyakazi wote kwa kuwa na mafanikio makubwa na kuifanya DCB kuwa benki ya kuigwa mfano.“Ndugu wanahisa napenda kutumia hadhara hii kutoa pongezi kwa kipekee kwa Bodi na Manejimenti ya DCB kwa kuweza kufanikisha zoezi la uuzaji wa Hisa kwa kuvuka lengo ambalo na mimi kwa bahati nzuri nikaingia katika dirisha na pia kwa kufanikisha benki kuorodheshwa hisa zake kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), nadhani kufanya hivi kunatoa fursa kwa wananchi na wawekezaji kwa ujumla kuendelea kunufaika na benki hii.“Kwa niaba ya ofisi ya Rais TAMISEMI nafarijika sana kuona mshikamano uliopo kati ya wanahisa waanzilishi, wanahisa wapya na wawekezaji wengine, kwa ujumla katika kufika kwenu hapa ni kielelezo tosha kuwa mna nia ya dhati kuwekeza katika benki yenu kwa lengo la kukuza mtaji wake na kuwapa faida kubwa kupitia ongezeko la thamani ya hisa na gawio la kila mwaka”, alisema Naibu Waziri Kandege.Alizipongeza manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo alisema kimsingi ndiyo wamiliki wake wakubwa na wametoa mchango mkubwa katika kufikia mafanikio hayo.Naibu Waziri huyo alisema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa mchango kwa benki hiyo kwa kuongeza jitihada za makusudi zenye lengo la kukuza vyanzo vya mapato vya manispaa na halmashauri zake na kuongeza ushiriki wa wananchi kupitia DCB kwa lengo la kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii.“Serikali kwa ujumla itaendelea kutekeleza wajibu wake kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa kuhuwisha sera na sheria zenye lengo la kuboresha mazingira yatakayowavutia wawekezaji wa fedha kupitia mabenki. Imani yangu kubwa Benki ya DCB itatumia fursa hiyo kwa kuwa mshindani mahiri,” aliongeza Naibu Waziri.Akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Prof. Lucian Msambichaka alisema, mafanikio ya zoezi la uuzwaji wa Hisa za DCB hatimaye kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ni ishara kuwa benki hii ina mvuto na inafanya kazi vizuri.Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa aliwahakikishia wanahisa wa DCB kuwa benki yao itaendelea kufanya vizuri kutokana na mikakati kabambe waliyojiwekea hivyo kufanya uwekezaji wao uwe na tija.Naye Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ambazo ndio wanahisa wakubwa wa benki hiyo, wana imani kubwa na utendaji wake na akaupongeza uongozi wa DCB kutokana kwa namna wanavyofanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika benki hiyo.