Mkazi wa mjini Singida akiwa amenunua mahitaji yake na kubeba katika
mfuko mbadala au halisi kama ambavyo inaitwa ikiwa ni katika utekelezaji
wa katazo la mifuko ya plastiki.
Mwananchi wa mjini Singida akionesha mfuko mbadala ambao anautumia
kubebea bidhaa anazonunua dukani akitii sheria bila shuruti ambayo
imeanza kutekelezwa Juni mosi.
Mifuko mbadala inayoagizwa kutumika badala ya ile ya plastiki kama
inavyoonekana wakati wa utoaji elimu kuhusu katazo la mifuko ya plastiki
sambamba na oparesheni ya kukagua kama bado ipo kwenye maeneo
mbalimbali mjini Singida.
Mfanyabiashara wa nyama akionesha mifuko mbadala anayoitumia
kuwafungashia kitoweo hicho wateja kufuatia katazo la mifuko ya plastiki
ambayo ilizoeleka kutumika.
Mifuko mbadala ikiwa imetundikwa kwa ajili ya kuhudumia wateja katika soko la mjini Singida ambapo kikosi kazi kilichoundwa na Serikali kikipita kukagua iwapo mifuko hiyo ikiendelea kutumika ama la.
**************************************
Oparesheni ya kukagua mifuko ya plastiki na utoaji elimu kuhusu katazo la mifuko ya plastiki linaloratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais limekwenda vizuri katika Mkoa wa Singida.
Hayo yamebainishwa na Mkaguzi wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati, Mhandisi Boniphace Guni wakati wakati wa oparesheni hiyo maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Zoezi limekwenda vizuri na tunamshukuru Naibu Waziri (Mhe. Mussa Sima) kwa kuhamaisha na kutoa elimu na tumeona wananchi wamepata uelewa na adhabu yote hii ni kuwafanya waache kutumia mifuko hii iliyokatazwa kisheria”. alisema.
Guni alisema tathmini inaonesha na kuwa NEMC ambayo ni mojawapo ya wajumbe wa kikosi kazi wameshirikiana na maafisa kutoka Manispaa ya Singida wameshuhudia mifuko hiyo ikisalimishwa baada ya agizo la Serikali.
Aliongeza kuwa jamii kutokana na elimu iliyotolewa wananchi wameweza kupata uelewa wa madhara ya kutumia mifuko ya plastiki na kuwa ni hatari kwa afya na mazingira.
Aidha, Mkaguzi huyo alisema wananchi wametambua fursa za kuzalisha mifuko mbadala ambayo imekuwa inahitaji kwa kiwango kikubwa baada ya kupigwa marufuko kwa mifuko ya plastiki.
&qu t;Mhandisi Guni aliishukuru Serikali kwa kwa kutunga sheria ambazo zinasaidia kulinda afya za wananchi ingawa wapo wasiopendi kuifuata, jukumu letu ni kuendelea kutoa elimu na inapobidi kutoa adhabu inapoonekana kutoheshimiwa”alisisitiza. Kwa upande wake Afisa Mazingira kutoka Manispaa ya Singida, Arafa Halifa alisema wananchi wamekuwa na muitikio mzuri katika kutekeleza katazo hilo.
Halifa alibainisha kuwa kuna wafanyabiashara wanane ambao
walisalimisha mifuko hiyo hivi karibuni huku mwingine akisalimisha shehena kubwa katika ofisi za manispaa hiyo.
Alisema zoezi kubwa linaloendelea kwa sasa tangu sheria zianze kutumika Juni mosi ni kuzunguka kaika maduka , masoko na sehemu zingine za biashara na kuona kama katazo linatekelezwa.
“Bado pia tunaendelea kutoa elimu na kusimamia sheria kama haifuatwi basi tunatekeleza adhabu na hapa kama unavyoona sisi manispaa tumeunda kikosi kazi kikiwa na maafisa mbalimbali wakiwemo wa biashara, mazingira, maendeleo ya jamii na mwanasheria”. alisema.
Afisa mazingira huyo alisema pamoja na mambo mengine amekuwa akisikia kilio cha wananchi kuomba kasi ya uagizaji mifuko mbadala iwe kubwa kwani kuna mahitaji makubwa.