Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (aliyesimama) akiongea na Wakaguzi wa Kemikali (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia ulioandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika leo katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar es Salaam. Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara za Huduma za Ubora wa Bidhaa, Sabanitho Mtega, Maendeleo ya Biashara, George Kasinga, Usimamizi wa Kemikali, Daniel Ndiyo na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba, Elias Mulima.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Kemikali, Daniel Ndiyo
(aliyesimama), akizungumza na Wakaguzi wa Kemikali (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (wa tatu kulia) kufungua Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Kemikali leo.
Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia wakimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo.
Mkaguzi wa kemikali na Maabara za Kemia kutoka Maabara ya Kanda ya Kaskazini, Jovitus Mukela (aliyesimama), akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakaguzi mara baada ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufungua Mkutano huo.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (aliyekaa katikati), akiwa pamoja na Wakurugenzi na Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali mara baada ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi hao uliofanyika Ukumbi wa Baraza
la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Dar es Salaam.
************************************
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amewasisitiza wakaguzi wa
kemikali na maabara za kemia kuzingatia ueledi, uadilifu na uaminifu katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mkemia Mkuu wa Serikali amezungumza hayo leo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka Mamalaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali uliofanyika Baraza la Maaskofu, Kurasini, Dar es Salaam.
Serikali imetupa majukumu ya kusimamia Sheria ya Mamlaka ya Maaabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani na Sheria ya Vinasaba vya Binadamu hivyo tunapaswa kuzingatia ueledi, uadilifu, uaminifu na upendo ili kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.
“Tutambue Serikali yetu imejielekeza katika kujenga uchumi wa viwanda na inajitahidi kuwekeza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ikiwemo wanaojihusisha na kemikali, hivyo tunapotekeleza majukumu yetu tunapaswa kuelewa uelekeo huo wa Serikali na kufanya maamuzi kwa wakati na haraka ili kutokwamisha wadau wetu huku tukizingatia Sheria” alisema Mafumiko.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali alisema Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti inawapongeza wakaguzi hao kutokana na kazi kubwa wanayofanya na inawahamasisha kuboresha zaidi huduma kwa wadau kwa kufuata Sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza kama watumishi wa umma.
“Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti inatambua mchango mkubwa wa wakaguzi katika kusimamia Sheria na kuingiza maduhuli ambayo taasisi inatumia katika kuboresha huduma na kujiendesha. Tunatambua changamoto zipo na tunaendelea
kuzifanyia kazi kama kuongeza watumishi na vitendea kazi. Tuna maeneo ya msingi ya kuyawekea kipaumbele hasa kwenye uwekezaji wa mitambo ya kisasa ya maabara na teknolojia ili kuwawezesha wakaguzi kutoa huduma bora na za haraka kwa
wadau. Tufanye kazi kama familia ili kuweza kutekeleza majukumu yetu kwa mafanikio.” Alimaliza.
Akitoa neno la shukrani, Mkaguzi wa Kemikali, Bw. Jovitus Mukela alimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko kwa nasaha nzuri za ufunguzi wa Mkutano huo.
Kwa niaba ya wakaguzi wenzangu tunakushukuru sana kwa nasaha na maneno mazuri uliyotuambia maana pia yanatukumbusha majukumu yetu na napenda kuwaomba wakaguzi wenzangu kuzingatia yale yote yaliyozungumzwa na kushirikiana kutoa huduma nzuri, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeitendea haki Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, sisi wenyewe na nchi kwa ujumla.” alisema Mukela.