MAMA aliyejifungua watoto mapacha wanne Radhia Solomon (24) mkazi wa Chemchemi Magomeni jijini Dar es Salaam na kutelekezwa na mmewe kwa madai ya kukwepa majukumu leo Juni 3, 2019 amewasili bungeni jijini Dodoma ambapo bunge limeridhia kila mbunge wa kiume kumchangia Sh. 100,000 na kila mbunge wa kike kumchangia Sh. 50,000 fedha ambazo zitatumika kumsaidia kujikimu na kuwatunza watoto hao hivyo kufanya jumla ya Tsh milioni 32,050,000.
Akizungumza leo Juni 3, bungeni jijini Dodoma Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema jukumu la utunzaji wa watoto ni la kila jamii hivyo bunge limeamua kufanya mchango huo kwa wabunge ili kumsaidia mama na watoto huku akiwaasa wanaume kuacha tabia ya kutelekeza familia zao.
Mama huyo alijifungua watoto hao Januari 8, 2019, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, ambao ni watoto wa kike wawili, Faudhia na Fardhia, na wa kiume wawili, Suleiman na Aiman.
Kwa mujibu wa mama huyo, matunzo ya watoto hao kwa siku kuwanunulia maziwa, yaligharimu Sh. zipatazo 40,000 kwa siku, hali iliyomfanya kuzorota kiafya na hatimaye kukimbiwa na mumewe.