********************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
JESHI la polisi mkoani Pwani ,kupitia kikosi cha usalama barabarani limefanikiwa kukusanya zaidi ya sh.milioni 89.3 kutokana na makosa ya usalama barabarani na madai ya serikali yapatayo 2,266 .
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,alisema jeshi hilo kupitia kikosi hicho lilifanya operesheni maalum yenye lengo la kudhibiti matumizi mabaya ya barabara.
Wankyo alieleza, katika operesheni hiyo walikamata makosa ya mwendokasi,kupita magari mengine sehemu isiyoruhusiwa na kupakia mizigo kupita kiasi.
Makosa mengine ni pamoja na madereva walevi na ukaguzi wa magari yanayobeba wanafunzi na pikipiki ambapo jumla ya makosa 1,680 yaliandikiwa faini na kukusanywa milioni 50.4.
“Madai ya serikali ni 586 ambapo makusanyo ni sh.milioni 38.938.5 jumla makosa na madai 2,266 na makusanyo milioni 89.338.5″alifafanua Wankyo.
Hata hivyo ,Kamanda huyo alisema ,katika operesheni hiyo makosa ya magari na pikipiki yalikamatwa na watuhumiwa walionywa na wengine kutozwa faini ya papo kwa papo na magari yaliyokuwa na madai ya serikali kulipia madai.
Wankyo alichukua fursa hiyo, kutoa rai kwamba,askari wa usalama barabarani wataendelea kutandazwa na wapo kazini muda wote ili kuhakikisha hakuna chombo cha moto kitakachofanikiwa kupita ndani ya mkoa huo bila kukaguliwa.
Alibainisha kuwa,watumiaji wa barabara za mkoa huo wasichukulie kigezo cha kumalizika kwa operesheni hiyo kukiuka sheria za usalama barabarani kwani atakaefanya uzembe wa makusudi atachukuliwa hatua za kisheria na kupigwa faini lengo likiwa kupunguza ajali mkoani humo