CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kusini Unguja kimewataka Viongozi na Watendaji wa Chama wa Ngazi za Matawi hadi Majimbo katika Wilaya hiyo kufanya Ziara za mara kwa mara katika Taasisi mbali mbali za Serikali ili kubaini Changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa huduma bora kwa Wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo Ndugu Abdulaziz Hamad Ibrahim katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Vituo vya Afya vilivyopo katika Jimbo la Paje Unguja.
Amesema endapo Viongozi wa Ngazi hizo wataendeleza Utamaduni wa kufanya ziara hizo itasaidia kupunguza Changamoto zilizipo katika Sekta mbali mbali za Utoaji Huduma kwa Wananchi zifanyiwe kazi na Mamlaka husika.
Alisema kupitia ziara hiyo ya Siku mbili katika Vituo vya Afya vya Majimbo ya Makunduchi na Paje imeleta mafanikio makubwa kwani changamoto zilizobainika kukwamisha upatikanaji wa Huduma za Afya zitawasilishwa kwa Mamlaka husika ili zitatuliwe kwa lengo la kuleta ufanisi.
Alisema CCM inatekeleza Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2015/2020 kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha Wananchi wa Mijini na Vijijini wanapata huduma bora za Afya na Mahitaji mengine kwa viwango vinavyostahiki.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Abdulaziz alieleza kwamba kazi hizo za Usimamizi wa Ilani zitakuwa endelevu ili kuandaa mazingira rafiki ya upatikanaji wa Ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo imefanyika katika Vituo vya Afya vya Paje,Bwejuu,Michamvi na Mungoni.