Home Mchanganyiko WAZIRI LUGOLA AIPA MAJUKUMU BODI MPYA USIMAMIZI MIRADI YA MAGEREZA

WAZIRI LUGOLA AIPA MAJUKUMU BODI MPYA USIMAMIZI MIRADI YA MAGEREZA

0

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akitoa maelekezo kwa wajumbe wa Bodi mpya ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, kabla ya kuizindua Bodi hiyo, jijini Dodoma, leo. Wapili kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, akizungumza kabla ya Waziri wa Wizara hiyo, Kangi Lugola (wapili kushoto) kuizindua Bodi mpya ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, jijini Dodoma, leo. Wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Phaustine Kasike, akitoa historia fupi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi hilo, kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) kuizindua Bodi hiyo, Jijini Dodoma, leo. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.

Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza, Meja Jenerali Mstaafu, Raphaeli Muhuga, akitoa neno la shukrani baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo, jijini Dodoma leo. Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (wapili kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu (wapili kulia), Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi mpya ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza, baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo, jijini Dodoma leo.

Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

………………..

Na EZEKIEL NASHON, DODOMA.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola ameiagiza bodi mpya ya Shirika la uzalishaji mali la Jeshi la Magereza nchini, ndani ya miezi miwili ihakikishe maeneo yote yaliyochini ya miliki ya Jeshi hilo kuhakikisha yamepimwa na kuwa na hati miliki pamoja na nyaraka zote.

Sambamba na hilo bodi ihakikishe inakuja na mipango thabiti ya kuimarisha shirika hilo, ikiwa ni  pamoja na  Jeshi la Magereza linajitegemea kwa kila kitu bila kutegemea Serikali kuu.

Waziri  Kangi  Lugola umetoa maagizo hayo  Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa bodi ya Shirika la uzalishaji mali la jeshi la Magereza iliyoundwa kusimamia miradi yote iliyochini ya Shirika hilo ili iweze kuleta tija kwa Jeshi na jamii.

Amesema bodi hiyo  ihakikishe ndani ya miezi miwili kwa kushirikiana na wataalamu ndani ya Jeshi hilo maeneo yote yanayomilikiwa na jeshi la magereza yawe yemepimwa na kuwa na hati miliki halali, kwa sababu kumekuwa na migogoro mingi katika  maeneo hayo kwa sababu hayana hati miliki na kushindwa kuendelezwa.

“Niwaagize bodi mpya ndani ya miezi miwili muhakiki mnakuja na mpango mkakati wa kuhakikisha shirika hili linainuka kutoka hapa lilipo na kufikia kujitegemea kwa kila kitu bila kutegemea hata senti moja  kutoka serikali kuu”,

“Maeneo mengi ya magereza hayaendelezwi na niliambiwa kuwa shida ni kwamba maeneo mengi hayana hati miliki sasa niagize bodi hii mhakikishe maeneo hayo yanapimwa na kuwa na hati miliki pamoja na nyaraka” amesema Lugola.

Ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inatatua changamoto zote ambazo zinaikabili shirika hilo ambazo  zilikuwa zinasababisha shirika hilo kuto kuendelea na kuleta tija  kama malengo ya kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa mahabusu.

Ameagiza maeneo yote yanayomilikiwa na jeshi la magereza ambayo yatakuwa hayatumiki kwa matumizi yoyote yapandwe miti na kuhakikisha kila mfungwa katika magereza apande miti ya kuzalisha mbao ili isaidie katika viwanda vinavyoanzishwa na shirika hilo.

Pia ameitaka bodi  hiyo kuja na suruhu ya kuhakikisha taasisi zote zinazodaiwa na shirika hilo ambayo kwa sasa deni hilo linafikia shilingi bilioni 6.45,  amesema fedha hizo zikipatikana zitasaidia kuinua shirika hilo.

Kwa upande wake kamishna wa Jeshi la Magereza Nchini Faustine Kasike amesema shirika hilo lipo chini ya jeshi la magereza na lilianzishwa mwaka 1983 kwa mujibu wa sheria ya bunge ya mashirika na 23 ya mwaka 1974.

Amesema shirika lilianzishwa kwa lengo la kujiendesha kiuchumi na kibiashara baada ya miradi ya jeshi la magereza iliyokuwa ikiendeshwa kwa kutegemea fedha za serikali  kushindwa kujiendesha  kutokana na fedha hizo kutokufika kwa wakati.

Nae Katibu mkuu wa Wizara hiyo Jacob Kingu amesema kuzinduliwa kwa bodi hiyo ni historia kwani mda mrefu sana shirika hilo limefanya kazi bila ya kuwa na bodi na kusababisha kusuasua katika utendaji kazi wake.

Amesema katika Magereza kumi(10) ya kimkakati yaliyotengwa ametembelea Magereza saba(7) amesema hayo yote yamefanya vizuri, katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika magereza hayo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi hiyo Meja Jenerali mstaafu Raphael Muhuge, amesema bodi hiyo itatimiza majukumu yote iliyopewa na kuhakikisha inasimamia shirika hilo kikamilifu ili kuleta tija, ameahidi kuhakikisha shirika hilo linatoa gawio kwa serikali.

“Ni kuhakikishie mheshimiwa bodi hii itafanya kazi kwa ueledi mkubwa na kuhakikisha linaleta tija kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kutimiza majukumu yote iliyopewa, na nikuhakikishie tutahakikisha shirika hili linatoa gawio kwa serikali”, amesema.