Home Mchanganyiko Taswa FC Yawashukuru Waandaaji wa Ndondo Cup

Taswa FC Yawashukuru Waandaaji wa Ndondo Cup

0

Na Mwandishi wetu

Dar es Salaam. Uongozi wa timu ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa FC) umewashukuru  waandaaji wa mashindano ya Ndondo Cup pamoja na kushindwa kuingia  katika  hatua inayofuata.

Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa wamejifunza mengi katika mashindano hayo na kuahidi kushiriki tena msimu unaofuata baada ya kuwajengea wachezaji moyo wa kujiamini katika mashindano yam waka huu.

Majuto alisema kuwa lengo la Taswa FC lilikuwa kutoa changamoto kwa timu nyingine pamoja na ukweli kuwa wanafanya mazoezi mara moja tu kwa wiki tofauti na timu nyingine.

“Tumeonja ladha ya mashindano pamoja na kushika nafasi ya tatu katika kundi letu. Tumethubutu kushindana na kupanua wigo wa timu yetu na kuingia katika historia mpya, sasa tunarejea katika majukumu yetu ya kuyatangaza mashindano kupitia kalamu zetu,” alisema Majuto.

Alisema kuwa kitendo cha waandaaji  waandaaji kuhakikisha kila mechi inakuwa na daktari ambaye hutoa huduma kwa majeruhi wa timu zote kimewafurahisha sana na kuwataka waandaaji wengine kuiga mfano huo.

“Tumecheza mechi zote bila kukosa. Hii ni historia kwetu, kwani kuna timu za madaraja ambazo zimeshindwa kumaliza mashindano na kufungwa mabao mengi zaidi yetu, kwetu sisi historia, kwa sasa tunaweza kuyazungumzia mashindano kwa undani zaidi kwani tunayajua vilivyo. Katika shughuli yoyote changamoto hazikosekani,  Taswa FC  inawaomba waandaaji kutumia changamoto kama njia ya kupata mafanikio,” alisema.

Alifafanua kuwa hata wao (Taswa FC) walipata changamoto nyingi, lakini kubwa kitendo cha makipa wao kuogopa mechi na kujiamulia kutofika uwanjani.

“Tumewachukulia hatua za kinidhamu pamoja na kuwasimamisha kwa muda usiojulikana. Si wazalendo kwa timu yetu. Wachezaji na viongozi wamepitisha adhabu hiyo mara baada ya mechi na Ukwamani na kufungwa mabao 2-0,” aliongeza Majuto.