Home Siasa UWT ZANZIBAR WAPATA MAFUNZO YA UONGOZI

UWT ZANZIBAR WAPATA MAFUNZO YA UONGOZI

0

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

VIONGOZI wa Ngazi mbali mbali za Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Tanzania Mkoa wa Magharibi wametakiwa kuendeleza Utamaduni wa kuzungumza changamoto zinawakabili Wanachama wa Umoja huo pamoja na Chama kwa ujumla pindi wanapotembelewa na Viongozi mbali mbali katika Majimbo.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Ikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar Ndugu Catherini Peter Nao wakati akifungua Mafunzo ya kuwajengea Uwezo  Viongozi wa UWT ngazi za Wadi hadi Wilaya katika Mkoa Magharibi yaliyofanyika  katika Ofisi za Umoja huo Kiembe Samaki Unguja.

Ndugu Catherine alisema baadhi ya Viongozi wa Kamati hizo hawasemi changamoto zilizopo katika maeneo wanayoyaongoza hivyo kusababisha kuwepo na matatizo yanayoweza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa haraka na Viongozi wa Chama na Serikali.

Alisema tabia ya baadhi ya viongozi hao kuwa kimya na kutokuwa wabunifu wa kusoma alama za nyakati katika masuala mbali mbali ya Kiutendaji ndani ya UWT inakwamisha shughuli za Kiutendaji .

Alisisitiza suala la ushirikiano katika masuala ya kiutendaji ili kazi mbali mbali za UWT ziweze kwenda sambamba na matakwa ya Katiba na Kanuzi za Umoja huo na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.

Katika maelezo yake Bi.Catherine aliwataka Viongozi hao kutojihusisha na masuala ya makundi yasiyofaa ya kusaka Wagombea Urais,Ubunge,Uwakilishi na Udiwani kabla ya muda uliopangwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2017,  pamoja na miongozo na Kanuni mbali mbali za Chama.

Pamoja na hayo aliwakumbusha Viongozi hao kuwa kazi kubwa iliyopo mbele yao kwa sasa ni kujipanga vizuri ikiwemo kuongeza Wanachama wapya ndani ya CCM ambao ndio Mtaji madhubuti wa Kisiasa utakaoweza kufanikisha Ushindi wa CCM mwaka 2020.

Kupitia Mafunzo hayo pia aliwambia kwamba mwaka 2019 ni muda wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara ambao utakuwa ni kipimo halisi cha maandalizi ya ushindi wa 2020 ,hivyo kila Kiongozi wa Umoja huo ajipande kuwamasisha Wanawake wajitokeze kwa wingi wakati utakapofika kuwania nafasi za Uongozi na kuwachagua Wagombea wa CCM.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi Zainab Ali Maulid amesema kwamba lengo la Mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi hao majukumu yao ikiwemo mipango endelevu ya kufanikisha Ushindi wa CCM wa mwaka 2020.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Viti Maalum kupitia Mkoa wa Magharib ambaye pia ni Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar  Mhe.Amina Idd Mabrouk alisema Mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuwajengea uwezo imara Wanawake waweze kupata maendeleo endelevu katika Nyanja za Kiuchumi,Kisiasa na Kijamii.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuwaamini Wanawake kwa kuwateuwa katika nafasi mbali mbali za Uongozi ambazo wamekuwa wakizitendea haki kwa kutekeleza majukumu wanayopewa kwa ufanisi.

Mafunzo hayo elekezi ya siku moja kwa Viongozi wa UWT kuanzia ngazi za Wadi hadi Wilaya za Umoja huo yameandaliwa na Wawakilishi na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Magharibi Unguja.