Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizindua mpango wa natumizi bora ya ardhi kwa viijiji 226 vinavyopitiwa na Bomba la Mafuta katika kijiji cha Sojo kata ya Igusule wilaya ya Nzega mkoani Tabora, kulia kwa Lukuvi ni Naibu Waziri Nishati Subira Mgalu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi , Naibu Waziri Nishati Subira Mgalu na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri wakicheza ngoma wakati wa uzindizi mpango wa natumizi bora ya ardhi kwa viijiji 226 vinavyopitiwa na Bomba la Mafuta katika kijiji cha Sojo kata ya Igusule wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Picha na Wizara ya ardhi.
****************************************
Na Munir Shemweta, NZEGA
Wananchi wanaoishi vijiji linakopita Bomba la kusafirisha Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanzania sasa watanufaika na mradi huo kufuatia Serikali kutangaza mradi wa kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 226 linapopita bomba hilo.
Aidha, ilielezwa kuwa wakati wa utekelezaji mradi wa kupanga matumizi bora ya ardhi mwananchi hawatatozwa gharama yoyote na wale ambao maeneo yao yametwaliwa watalipwa fidia.
Hayo yalibainishwa tarehe 25 Mei 2019 katika kijiji cha Sojo kata ya Igusule wilaya ya Nzega mkoani Tabora na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakati wa uzinduzi Mradi wa Upangaji Matumizi bora ya Ardhi katika vijiji vinavyopitiwa na bomba la kusafirisha Mafuta ghafi -EACOP alipozungumza na wananchi wa kijiji hicho kuwaelezea mpango wa Wizara yake kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuendana na fursa za kiuchumi.
” Vijiji vyote 226 ambavyo Bomba la Mafuta linapita ardhi yao itafanyiwa matumizi bora ya ardhi ili kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo” alisema Lukuvi.
Akiwa na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu na baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi na Maliasili Waziri Lukuvi alisema, uzinduzi uliofanyika ni kwa niaba ya vijiii 226 na wilaya 24 zilizoko katika mikoa nane inapopita bomba hilo na kubainisha kuwa fedha kwa ajili ya mpango huo zishatengwa.
Waziri Lukuvi alitoa onyo kwa wananchi watakaojipenyeza au kufanya maendelezo katika eneo la ekari 144 lililotwaliwa na serikali na kusema tayari picha ya anga imechukuliwa katika eneo lote litakalojengwa kituo wezeshi cha kuunganisha mabomba ya mradi.
Kwa mijibu wa Lukuvi, mradi wa upangaji matumizi ya ardhi katika viiji vinavyopitiwa na bomba la mafuta utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha wananchi wanaoishi maeneo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Dkt Stephen Nindi alisema kazi ya upangaji matumizi bora ya ardhi imeanza katika vijiji, miji na miji midogo inayopitiwa na bomba la kusafirisha mafuta ghafi ambapo kazi hiyo imeanza katika wilaya 13 kati ya 24 zilizopangwa kufanyiwa matumizi bora ya ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt. Nindi uandaji mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji hivyo unafanyika kwa sababu kuna fursa na kuanisha kuwa katika kijii cha Sojo pekee kiasi cha bilioni 600 zitawekezwa kwa kuwa kituo katika kijiji hicho itakuwa kituo kikuu cha kuunganisha mabomba na hivyo kutoa fursa za kiuchumi na kijamii hivyo wananchi wajiandae namna warakavyobua fursa.
Aidha, alisema upangaji matumizi bora ya ardhi utasaidia kuepuka migogoro ya ardhi ambapo kwa kiasi kikubwa mradi huo utahusisha wananchi na kusaidia ulinzi na usimamizi wa bomba la mafuta sambamba kulinda maeneo yenye rasilimali kama misitu na maeneo Oevu.
Meneja wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha Mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanzania Martin Tiffen alisema kazi kubwa ya kuunganisha mabomba ya mradi itafanyika kwa lengo la kupunguza joto itafanyika katika kijiji hicho na kubainisha kuwa mradi huo utaboresha miundombinu ya barabara ili wananchi wanufaike.
Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kwa upande wa Tanzania litapita katika mikoa nane ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Dodoma na Tanga sambamba na kujumuisha wilaya 24 na vijiji 226 ambapo vijiji 30 viko katika mkoa wa Tabora.