Na Ahmed Mahmoud,Arusha
Wafugaji zaidi ya 9,000 kutoka mikoa minne ya Arusha, Tanga, Mwanza na Dar es Salaam wanatarajiwa kunufaika na elimu juu ya ufugaji bora wa kisasa na wenye tija ambao utawawezesha kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza jana kwenye kikao cha kuweka mikakati namna ya kuwafikia wafugaji hao kupitia elimu kwa njia ya radio ,Afisa mradi kutoka shirika la Radio kwa wakulima (Farm Radio International ) Eliakunda Urio alisema kuwa, wamekuwa wakifanya kazi na wakulima pamoja na wafugaji katika maeneo ambayo mradi unakuwepo katika kuhakikisha wakulima na wafugaji wanafikia malengo yao kwa kupata elimu iliyo bora.
Urio alisema kuwa, wafugaji hao watakaonufaika wamekuwa wakifanya shughuli zao katika ufugaji wa ng’ombe, kuku, mbuzi na kondoo ambapo wataweza kupata elimu juu ya mifugo hiyo sambamba na matumizi sahihi ya dawa za kudhibiti magonjwa.
Alisema kuwa, wamefikia hatua ya kutumia vyombo vya habari kwani ni nyenzo muhimu inayoweza kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ugani inayowakabili wakulima na wafugaji nchini kwa kuandaa vipindi vinavyotoa fursa Kwa walengwa kuwasiliana moja Kwa moja na wataalamu.
Naye Afisa msaidizi kitengo cha radio shirika la radio kwa wakulima (Farm Radio International), Clara Moita alisema kuwa, elimu hiyo inatolewa kupitia mradi wa miezi sita wa afya ya mifugo ambapo wamekuwa wakitoa mafunzo kwa waandaaji wa vipindi kabla ya kuanza kutekelezwa Kwa vipindi hivyo Kwa wakulima.
Clara alisema kuwa,elimu hiyo ambayo wamekuwa wakitoa kwa wakulima na wafugaji kupitia radio imekuwa ikileta mafanikio makubwa kutokana na kuwafikia wakulima wengi hasa waliopo vijijini na Kwa wakati mmoja na hatimaye kuweza kuongeza pato kutokana na kufuga na kulima kisasa zaidi.
Naye mfugaji wa kuku kutoka Nyamagana mkoani Mwanza, Betty Masumbigana alisema kuwa, wamekuwa wakikabiliana na changamoto nyingi katika ufugaji wao ikiwemo magonjwa yanayoshambulia mifugo mara Kwa mara, ambapo kupitia vipindi hivyo wameweza kuona manufaa makubwa kutokana na kupata ushauri namna ya kufuga kutoka Kwa wataalamu waliobobea.
Alisema kuwa, kupitia vipindi hivyo vimeleta matokeo chanya ambayo kwa asilimia kubwa yameanza kuziba pengo lililopo baina ya wakulima, wafugaji na watalaamu wa ugani.