****************
Na Khadija Khamis – Maelezo 22-5-2019
Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar Dk. Hussein Shaaban amewataka wadau mbali mbali kujiunga na mfumo wa usajili wa kielectroniki ili kuwarahisishia wananchi kupata uthibitisho wa utambulisho kwa urahisi .
Hayo aliyasema huko katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil ,Kikwajuni Zanzibar wakati wa Mkutano wa namna ya kuwaunganisha Wadau wa sekta za Serikali na Binafsi katika mfumo wa vitambulisho .
Amesema Mfumo huu utasaidia kurahisisha huduma za uthibitisho wa utambulisho wa wananchi kwa haraka kwa utambulisho wa ukaazi, kizazi, kifo, ndoa na talaka .
Aidha alisema elimu itatolewa kwa wananchi kupitia katika vyombo vya habari na machapisho mbali mbali ili kuweza kupata ufahamu wa utambulisho huo na kutoa mashirikiano kwa taasisi hiyo .
Hata hivyo Mkurugenzi huyo ametoa onyo kwa wadau ambao watajiunga na Wakala wa Usajili na Matukio wa Kijamii kudhibiti taarifa za wananchi zisitolewe kiholela .
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Idrisa Kitwana Mustafa alisema mfumo wa utambulisho utasaidia kuondoa urasimu wa kupata huduma kwa wananchi.
Pia alisema mfumo huu unahitaji kulindwa hivyo wadau wapewe taarifa ambazo wanazozihitaji sio kupata taarifa zote za mwananchi kufanya hivyo kutasaidia kudhibiti taarifa zisitumike vibaya na kupoteza lengo lililokusudiwa
Aidha aliishauri taasisi husika kuchukuwa hatuwa kwa mdau yoyote ambae atagundulika anazitumia taarifa hizi visivyo na kuweza kumfungia huduma hiyo
“Imani yangu kwamba Wadau wote ni Wazanzibar wazawa wa Nchi hii watautumia mfumo huu wa kielectronik ili kuhakikisha dhana ya Teknolojia inafanikiwa kwa kiasi kikubwa na Wananchi wa Zanzibar wanapata fursa kutokana na utambulisho huo .”alisema Mkuu wa Wilaya huyo
Usajili wa utambulisho kwa Zanzibar ulianza 1909 kwa kusajili taarifa za wananchi katika mfumo wa kizamani ambao unachukuwa muda mrefu hadi kukamilika tofaui na mfumo huu wa sasa .