Home Mchanganyiko HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YAANZISHA HUDUMA MAALUMU YA UCHUNGUZI WA SARATANI...

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA (BMH) YAANZISHA HUDUMA MAALUMU YA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI

0

Mashine (Mammography) ya uchunguzi wa ugonjwa wa saratani ya Matiti.

Mtaalam wa Radiolojia Mr Henry Mwansasu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa akimchunguza mgonjwa kwa kutumia mashine (ultrasound).

……………….

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kupitia kliniki yake ya kinamama wajawazito na uzazi imeanzisha huduma maalumu ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi (Cervical Cancer) kwa siku za Jumanne na Alhamisi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinamama na Uzazi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt, Caroline Damian, anasema BMH imeanzisha huduma hiyo ya bure ya uchunguzi wa saratani kutokana na kuongezeka kwa tatizo.

“Zaidi ya asilimia 80 ya wanaokuja hospitalini kwa ajili ya matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi, wanakuja katika hatua za mwisho za ugonjwa. Ndio maana tumeona umuhumu wa kuanzisha uchunguzi wa bure ili kubaini tatizo katika hatua za awali,” alisema.

Alisema saratani ya mlango wa kizazi inasabibishwa na kirusi cha binadamu cha Papilloma (Human Papilloma Virus), akibainisha kuwa kirusi hicho kinachangia kwa asilimia 99 ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa upande wake, Dkt Caroline Mrema, ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ametaja tiba za saratani kuwa ni pamoja na upasuaji katika hatua za awali za ugonjwa huo, mionzi na dawa kwa kutumia dripu.

“Tiba hizi hazitolewi zote kwa wakati mmoja kwa mgonjwa. Bali hutolewa kutokana na hatua za saratani, afya ya mama na umri wake,” alisema.

Akitolea ufafanuzi juu ya tiba ya mionzi, Dkt Mrema, alisema kumekuwa na fikra potofu juu ya tiba ya mionzi kuwa ina madhara, akisema tiba hii haina madhara wala haisababishi kifo kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodhani.