Wadau wa Bima pamoja na watu wa Mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Bima hapa nchini(TIRA)wakipata picha ya pamoja leo katika mkutano wa uzinduzi wa tuzo uliofanyika katika ofisi zao zilizopo jijini Dar es Salaam.
*********************************
NA EMMANUEL MBATILO
Ili kuimarisha taswira ya soko la Bima nchini na kuongeza uhitaji wa huduma hiyo kwa wananchi, Mamlaka ya usimamizi wa shughuli za Bima hapa nchini (TIRA) kushirikiana na wadau wa sekta hiyo wameamua kutambua na kutoa tuzo kwa makampuni pamoja na watu binafsi ama bidhaa za bima zilizofanya vizuri katika maeneo mbalimbali.
Tuzo hizo ambazo zinatarajiwa kutolewa Septemba 27 mwaka huu, zimelenga kuwashirikisha wananchi katika mchakato huo kwani wao ndio walengwa wa huduma zitolewazo na taasisi za Bima na hata hivyo zitakuwa zikitolewa kwa kila mwaka.
Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar Es Salaam katika ufunguzi wa tuzo hizo, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware amesema kuwa lengo kubwa la tuzo za umahiri wa Bima ni pamoja na kuendeleza uweledi taaluma ya bima na soko la bima kwa kubainisha, kuthamini, kutambua na kutoa tuzo za umahiri kwa kampuni ama bidhaa zilizofanya vizuri katika soko la Bima kwa kuzingatia vigezo.
Aidha Dkt. Saqware amesema kuwa uzinduo huo ni katika kuendeleza ajenda ya mamlaka ya Bima ya kupanua uwigo wa upatikanaji wa huduma za Bima nchini yaani Bima kwa wote, ikumbukwe hivi karibuni tulizindua kanuni za Mabenki kuuza Bima.
“Vigezo ambavyo tunaangalia ni pamoja na kuimarisha taswira ya sekta ya Bima nchini na kuongeza uhitaji wa bima, kuimarisha ukuaji wa sekta ya Bima na mchango wake katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi,Kubainisha, kutambua na kutunuku kampuni,mtu au bidhaa ya bima iliyotoa huduma nzuri hapa nchini, kukuza ubunifu katika sekta ya bima, kuonyesha umahiri wa soko la Bima nchini katika kushughulika na kukinga majanga yake na pia kuendeleza juhudi za serikali katika kukinga wananchi na mali zao”. Amesema Dkt.Saqware.
Pamoja na hayo Dkt. Saqware amesema kuwa matumizi sahihi na mazuri ya huduma za Bima huondoa umasikini kwa wananchi mmoja mmoja na kuongezea mitaji.