NA MWAMVUA MWINYI, PWANI
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde amewasihi vijana kuwa na uthubutu wa kuanzisha miradi midogomidogo ili kujikwamua kimaisha badala ya kuchukua muda mwingi kulalama vijiweni.
Aidha ameeleza,vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kutumia rasilimali kidogo walizonazo kwa kujiajiri kupitia ujasiriamali .
Aliyasema hayo alipotembelea mradi wa ufugaji wa kuku wa kijana mjasiriamali ,Robert Lugala maarufu kama Robi One uliopo eneo la Visiga Madafu ,wilayani Kibaha.
“Kijana huyu ni mfano, huu ni mfano mzuri kwa vijana wengine kwani mbali ya kujiajiri pia wanaajiri vijana wengine na wanapaswa kuacha kulalamika na kushinda vijiweni bali wawe na uthubutu kwa vile vinavyowezekana kwa kuweka nia,” alitoa rai Mavunde.
Alifafanua, serikali inaunga mkono jitihada za vijana kama hao ambao wanafungua fursa za kukabiliana na changamoto kubwa ya ajira .
Naye Robert Lugala -Robi One alisema ,mradi huo uko hatua za mwisho kukamilika .
“Utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kufuga kuku wa nyama wapatao 20,000 kwa wakati mmoja,nitaanza na vijana 10 ambapo wasambazaji kuku watakuwa ni vijana wanaozunguka eneo hili kupitia vikundi watakavyokuwa wameviunda”alisema Lugala .
Lugala alisema ,malengo yake ya baadaye ni kuwa na migahawa midogomidogo mingi hapa nchi itakayouza nyama ya kuku kutoka kwenye shamba lake hilo lengo kuwapa watanzania lishe bora na kuongeza ajira.
Kwa upande wake mmoja wa vijana waliopata ajira kwenye mradi huo Ally Kamtema alimshukuru Lugala kwa kuanzisha mradi huo kwani utawapunguzia vijana changamoto ya upatikanaji wa ajira.