Bilionea wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Saniniu Kurian Laizer akizungumza kwenye harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Narakauwo ambapo zilipatikana shilingi milioni 39, kulia ni Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka.
***********************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
Bilionea wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Saniniu Kurian Laizer ameiasa jamii ya wafugaji nchini kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakisha kila kaya inakuwa na mhitimu mwenye elimu ya shahada ili kusaidia jamii hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Bilionea Laizer ameyasema hayo kwenye kijiji cha Narakauwo katika harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT) na kupatikana shilingi milioni 39.
Bilionea Laizer amesema jamii ya wafugaji inakabiliwa na changamoto nyingi lakini wakiwekeza kwenye elimu kwa kusomesha watoto wao changamoto hizo zitapungua kama siyo kumalizika kabisa.
Amesema endapo kila kaya ya jamii ya kifugaji itakuwa na mhitimu wa elimu mwenye shahada, maisha yao yatabadilika kwani kila jambo litakuwa linafanyika kitaalamu.
Amesema kutokana na uwepo wa elimu ya jamii hiyo wasomi watakuwa na uwezo wa kukabili changamoto mbalimbali zinazowakabili tofauti na sasa kwani uwezo wa kuzikabili unakuwa mdogo kwa sababu ya ukoefu wa elimu.
“Tuwekeze kwenye elimu kwa watoto wetu ili tupate wasomi watakaotuelimisha kufuga kitaalamu, kuwekeza katika taasisi za fedha, kuboresha miundombinu ya ufugaji ili kipindi cha ukame mifugo isiteseke na mengineyo,” amesema bilionea Laizer.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema suala la kuwekeza kwenye elimu halina mjadala hivyo jamii ya wafugaji itoe kipaumbele katika elimu.
“Hata kwenye biblia imeandikwa mshike sana elimu usimuache aende zake maana ni uzima wako na waislamu katika hadithi za mtume wao alisema itafuteni elimu hata kama ipo mbali hadi China,” amesema Ole Sendeka.
Pia, mbunge huyo amewataka wananchi wa eneo hilo kutouza ardhi yao kwani watasababisha kuendeleza migogoro ya ardhi inayorudisha nyuma maendeleo.
“Tunapaswa kutambua kuwa watu na mifugo inaongezeka na ardhi haiongezeki hivyo tusiuze ardhi kiholela ili kuepusha migogoro isiyo na tija,” amesema Ole Sendeka.
Hata hivyo, Diwani wa kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardadi) amewashukuru viongozi na wananchi walioshiriki kwenye harambee hiyo ya ujenzi wa kanisa.
“Kwenye harambee hii zimepatikana shilingi milioni 39 ambapo fedha taslimu ni shilingi milioni 29 milioni na ahadi shilingi milioni 10 zinazotarajiwa kutolewa wakati wowote kuanzia sasa,” amesema Mardadi.