Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea wakati akikagua mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe mapema leo, ambapo amesema serikali imefuta mkataba na Mkandarasi ya kampuni ya M.A.Kharafi & Sons iliyokuwa ikijenga chanzo cha mradi huo. Waziri Aweso katika ukaguzi wa mradi huo ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mgwira, pamoja na viongozi wengine.
****************************************
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Serikali imeamua kusitisha mkataba wa mkandarasi kampuni ya M.A.Kharafi & Sons aliyekuwa anajenga chanzo cha mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe kutokana na ucheleweshaji wa mradi wakati wananchi wanaendelea kukosa maji.
Mhe. Aweso ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Desemba, 2020 baada ya kukagua utekelezaji wa mradi na kuongeza kuwa kazi nyingine za mradi huo zitafanywa na Wizara lakini hatua zitachukuliwa haraka za kupata Mkandarasi mwingine atakayemalizia kazi zilizobaki za mfumo wa umeme.
“ Serikali itasimamia kuhakikisha kwamba Kampuni ya M. A. Kharafi & Sons inawalipa stahiki zao watumishi wote waliofanya kazi katika mradi. Sisi kama Serikali tunawaomba radhi wananchi wa Same, Mwanga na Korogwe kwa kuchelewa kupata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kupitia mradi huu” Mhe. Aweso amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inamtaka Mkandarasi mwingine katika mradi huo kampuni ya Badr East Africa Enterprises Ltd aongeze kasi ya utekelezaji wa kazi za mradi kuendana na Mikataba yake ili akamilishe kwa wakati kulingana na Mkataba na itakapofika mwezi Machi 2021 kwa sababu hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza.
Waziri Aweso ametoa agizo kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji nchini kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kuikamilisha kwa wakati kulingana na mikataba yao ili wananchi wanufaike kupata huduma ya majisafi na salama .
Serikali kupitia Wizara ya Maji inatekeleza mradi wa maji wa Same– Mwanga – Korogwe ambao unakadiriwa kugharimu shilingi 262 Bilioni na unatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 438,000.