Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza katika kikao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia (hayupo pichani) kilichojadili maendeleo ya Michezo nchini. Kikao hicho kilifanyika Desemba 23, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega akizungumza katika kikao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia (hayupo pichani) kilichojadili maendeleo ya Michezo nchini. Kikao hicho kilifanyika Desemba 23, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Bw. Wallace Karia akizungumza katika kikao cha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (hayupo pichani) pamoja na Shirikisho hilo kuhusu maendeleo ya soka nchini. Kikao hicho kilifanyika Desemba 23, 2020 Jijini Dar es Salaam.
**********************************************
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali itashirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF katika kuendeleza Michezo.
Mhe.Waziri Bashungwa ameyasema hayo Desemba 23, 2020 Jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na Shirikisho hilo akiwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega ambapo amesema kuwa ni lazima Serikali na Shirikisho hilo kuwa na Mpango Mkakati wa pamoja wa kuendesha michezo nchini.
“Serikali tuko tayari kushirikiana na TFF, Hivyo lazima shughuli zote za michezo za timu za taifa za ndani na nje ya nchi Serikali iwe na taarifa” Waziri Mhe.Bashungwa.
Mhe.Waziri Bashungwa ameongeza kuwa Shirikisho hilo lazima liweke kipaumbele kwenye michezo ya watoto wa shule za msingi na sekondari ili kupata wachezaji wazuri wa timu za Taifa.
Huku akieleza kuwa Serikali imetenga shule 56 kwa ajili ya kufundisha michezo lengo ni kuzalisha wanamichezo wengi na bira nchini.
“Nasisitiza utawala bora katika kuendesha michezo ikiwemo usimamizi madhubuti wa fedha zinazoingia TFF” alisema Waziri Bashungwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amesisitiza kuwa Shirikisho hilo lisimamie mchango wa soka katika kupata fedha za kuhudumia timu za Taifa.
“Ni lazima tuzo kwa wanamichezo zirejee na zipewe uzito unaostahili, lengo ni kutambua mchango wa wanamichezo katika Taifa letu” alisema Naibu Waziri Ulega
Naibu Waziri Mhe. Ulega amesisitiza kuwa TFF isimamie vilabu vinavyoshiriki Kombe la Mapinduzi kupeleka timu bora kwa heshima ya kombe hilo.
Mhe.Naibu Waziri amesisitiza pia uhamasishaji wa michezo kwa timu za Taifa ikiwemo uhamisishaji wa ununuzi wa jezi za timu ya Taifa.
Naye, Rais wa Shirikisho hilo Bw. Wallace Karia amesema kuwa Shirikisho hilo limeanza kutekeleza Ilani ikiwemo kuwa na Mpango Mkakati wa kuendeleza michezo pamoja na kuimarisha Utawala Bora.
Vilevile, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Bw.Alfred Kidau ameeleza kuwa maandaalizi ya kushiriki Kombe la CHAN yameanza ambapo timu zitaingia kambini Januari 2021.