******************************************
Eneo lolote linalotumika kwaajili ya kuendesha shughuli za kumuabudu Mungu halitatozwa kodi ya ardhi isipokuwa maeneo mengine ya taasisi za kidini yanayotumika kwa matumizi ya shughuli za kijamii kama vile shule, zahanati, vituo vya afya, maduka na nyumba za kupangisha kwa kuwa yatakuwa yanatumika kwa kuingiza kipato.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na viongozi wa madhehebu yote ya dini ndani ya wilaya ya Ilemela kusikiliza kero zinazowakabili na kisha kuzipatia ufumbuzi, kupokea ushauri, kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuwashukuru baada ya kuisha salama kwa zoezi la uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi oktoba mwaka huu ambapo amefafanua kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Mhe Dkt John Magufuli ni sikivu, yenye hofu ya Mungu na inatambua mchango wa viongozi wa dini katika maendeleo ndio maana imeondoa tozo kero kwa madhehebu ya dini ikiwemo kodi ya ardhi katika eneo linalotumika kwa shughuli za ibada
‘.. Zamani ile kodi ya nyumba ilikuwa inaangalia thamani ya nyumba inapigwa kwa asilimia, Ilikuwa ni kubwa sana lakini Mhe Dkt John Magufuli akasema hapana, kwenye maeneo ya kidini ilikuwa unalipia eneo lote bila kujali linatumikaje, Lakini sasa hivi na tumeelekeza kama wizara katika yale maeneo yenu ya taasisi za dini hasa kwenye majengo ya kuabudia tujue linachukua eneo gani, Hilo halidaiwi kodi, Lakini matumizi mengine unaweza kukuta eneo ni kubwa na kuna shule, zahanati, kuna duka, hayo yatadaiwa kodi ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula akawahakikishia ushirikiano viongozi hao katika kuhakikisha jimbo la Ilemela linakuwa kinara wa maendeleo sanjari na kukemea watumishi wasiokuwa waadirifu wanaosababisha urasimu katika zoezi la urasimishaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi kwani kitendo hicho kinaikosesha Serikali mapato na kinachelewesha maendeleo.
Kwa upande wake Mchungaji Dkt Jacob Mutashi kutoka kanisa la EAGT Kiloleli mbali kumpongeza Rais Mhe Dkt John Magufuli na Mbunge huyo kwa namna wanavyotatua kero za wananchi akamshauri kiongozi huyo kuendeleza utamaduni wake wa kutenga muda kabla ya kuanza kwa vikao vya bunge ili kuzungumza na viongozi hao wa madhehebu ya dini na kuiomba Serikali kuwatumia kama njia ya kufikisha ujumbe kwa jamii huku Shekh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke akipongeza kwa uamuzi wa naibu waziri kukutana na viongozi wa dini kwani ni viongozi wa chache wenye moyo wa kufanya hivyo pamoja na kumuahidi ushirikiano katika maendeleo.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula, Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu John Wanga aliyeambatana na afisa ardhi na mipango miji wa manispaa ya Ilemela Ndugu Shukran Kyando ambapo walitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyowasilishwa na kuahidi kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika masuala ya ardhi.