Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Manyara,
Joseph Mkirikiti alipomtembelea ofisini kwake jana.Waziri Gekul
yupo mkoani Manyara kwa ziara ya Kikazi.
Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi, Ukuzaji Viumbe Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Imani Kapinga
alipokuwa akimpa maelekezo Mwakilishi wa Kampuni ya XIN SI LU, Suvi Zeng (katikati) alipotembelea eneo la
ufugaji wa Samaki katika Mabwawa la Kampuni hiyo jana.
Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) akipokea samaki aina Sato kutoka kwa
Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi
alipotembelea eneo la Kampuni ya XIN SI LU kutoka China iliyowekeza
katika ufugaji wa Samaki kwenye Mabwawa Mkoani Manyara jana.
Na Mbaraka Kambona, Manyara
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi, Pauline Gekul amewataka wale wote wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia
sheria na taratibu kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa
watakaokamatwa.
Gekul alitoa onyo hilo
alipokuwa akiongea na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo jana.
Kwa mujibu wa Waziri Gekul
katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu
bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa
ushirikiano kwa serikali ili kukomesha vitendo hivyo.
“Hatutavumilia jambo hili
liendelee, Sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi
haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili
uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema Gekul.
Aliongeza kwa kusema kuwa
uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi
ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.
“Kwa kuwa mmeonesha nia ya
kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo
nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho
,” aliongeza Gekul.
Aidha, Waziri Gekul alisema
kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa
kutumia Vizimba na Mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza
ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu.
“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi
wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa
na Serikali kwa Vijana, Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye
utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa
ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la
ajira,” alisisitiza Gekul.
Katika hatua nyingine,
Gekul aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi
wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na
kukuza pato la Serikali.
“Hili litekelezwe haraka,
kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti
za mashine za elekroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya
serikali,” alifafanua.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Babati, Lazaro Twange alisema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri
wameyapokea na watayafanyia kazi kama ilivyoelekezwa ili sekta ya uvuvi mkoani
humo iweze kupiga hatua inayotarajiwa.
“Tutahakikisha wavuvi wote
tunawafikia kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili lakini vile vile wale
ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili serikali iweze kuwatambua na
kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” alisema Twange.
Mwenyekiti wa Wavuvi,
Halmashauri ya Babati, Iddi Hassani alisema kuwa watafanyia kazi maelekezo na
watahakikisha wanashirikiana na serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi
na wataendelea kupambana na uvuvi haramu ili kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya
uvuvi endelevu.