Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu OR TAMISEMI anayeshughulikia elimu Gerald Mweri akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Rais wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mwalimu Frank Mahenge akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link Abdulmalik Mollel akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa 15 wa wakuu wa shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA Mkutano unaofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.
Pichani ni baadhi ya Wakuu wa Shule za Sekondari hapa nchini waliohudhiria mkutano wa 15 unaowakitanisha wakuu hao kijadili mambo mbalimbali mkutano unaofanyika Jijini Dodoma.
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mheshimiwa Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Nne kuandika barua kwa Katibu Mkuu TAMISEMI mhandisi Joseph Nyamhanga kujieleza ni kwanini walishindwa kuwaruhusu wakuu w shule kuhudhuria mkutano wao wa mwaka.
Waziri Jafo, ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha wa wakuu wa shule za sekondari Tanzania bara (TAHOSSA) unaofanyika jijini Dodoma.
Amebainisha, kuwa mkutano kama huo ndiyo sehemu ambayo serikali inatumia kutoa maagizo kwa wakuu wa shule katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya kielimu katika maeneo yao.
Amesema, serikali ya awamu ya tano imetoa fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya elimu ambayo wasimamizi wakuu ni wakuu wa shule za sekondari hivyo ushiriki wao katika mkutano huo ni jambo la lazima.
“Kuna kiasi kikubwa cha fedha serikali imewekeza katika kuboresha miundombinu ya shule nchini na wasimamizi ni nyinyi wakuu wa shule hivyo uwepo wenu hapa na sisi serikali tunapata fursa yakutoa maagizo yetu lakini sasa kuna baadhi ya wakurugenzi wameshindwa kutoa vibali kwa wakuu wa shule” amesema Jafo.
Wakurugenzi, ambao hawakutoa ruhusa kwa wakuu wa shule za sekondari kwamujibu wa Jafo ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Kahama DC, Kologwe DC pamoja na Sikonge.
Kutoka na hali hiyo Waziri Jafo, amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga kuwachukulia hatua wakurugenzi hao haraka.
“Namwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Nyamhanga kuhakikisha wakurugenzi hawa wanatoa maelezo kwanini wameshindwa kutoa ruhusa, na hatua hizo zichukuliwe haraka”amesema.
Vile vile Jafo, amewaagiza wakurugenzi Halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha kuwa mwaka 2021, wanasimamia upimaji wa maeneo ya shule ili kupata hati miliki na kuondoa migogoro ya ardhi.
Amebainisha katika mwaka wa Fedha 2020/21 serikali imetenga zaidi ya Sh. bilioni 68 kwajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 2,088.
“Lakini pia tumetenga kiasi cha Sh. bilioni 42.3 kwajili ya ujenzi wa vyumba vya maabara ili kuwezesha vijana wetu wanaosoma masomo ya sayansi kujifunza kwa vitendo”amesema.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wakuu wa shule za Sekondari Tanzania Bara (TAHOSSA) Mwalimu Frank Mahenge, amesema mkutano huo ni wa 15, ambao hutumika kutathmini malengo waliyojiwekea na kushirikishana changamoto zilizopo ili kuzitatua.
Ameongeza kuwa “Changamoto nyingine ndugu mgeni rasmi ni kutokana na shule nyingi kukosa uzio hali inayosababisha utendaji kazi kwa walimu kuwa katika mzingira yasiyo rafiki pamoja na wanafunzi wao”amesema.
Hata hivyo, amesema kuwa moja kati ya majukumu ambayo TAHOSSA watafanya katika mwaka ujao ni kuwajengea uwezo walimu kwa kuanza na kanda ya kati na kusini.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link Abdulmalik Mollel, ambao ndiyo waratibu wa mkutano huo, amesema kuwa umekuwa na mabadiliko makubwa tofauti na miaka iliyopita.
Amesema, katika mkutano wa mwaka huu wamezialika Taasisi mbalimbali za elimu ili wakuu wa shule za sokondari wapate elimu ambayo wataifikisha kwa wanafunzi wao ikiwemo namna ya kufanya udahili kujiunga na vyuo vikuu.