Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega na Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi wakiangalia kazi za Sanaa zilizobuniwa na kutengenezwa na Wanafunzi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) pamoja na baadhi ya vyombo vya muziki walipofanya ziara katika taasisi hiyo Desemba 21, 2020 . Katika ziara hiyo Mhe. Waziri alitoa miezi mitatu kuanzia januari 2021 kwa taasisi hiyo kujitangaza ili ijulikane iweze kupata wanafunzi wengi wa fani hiyo.
*******************************************************
Na Shamimu Nyaki – WHUSM, Bagamoyo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ametoa miezi mitatu kuanzia mwezi January 2021 kwa Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kujitangaza, kupitia njia mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii ili wananchi wakijue na wajiunge kujifunza Sanaa ambayo ni njia mojawapo ya kujiajiri.
Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 21, 2020 Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani alipotembelea Chuo hicho pamoja na Naibu wake Mhe. Abdallah Ulega na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbbasi.
“Tumieni Vyombo vya Habari kutangaza maudhui yanayohusu Chuo hiki, ili muweze kupata wanafunzi wengi ambao watajifunza sanaa,” Mhe.Waziri Bashungwa.
Waziri huyo alisema, suala la ubunifu katika kutoa elimu ya Sanaa ni jambo la msingi hivyo ameitaka TaSUBa kutoa matangazo ya kozi wanazofundisha ili kusaidia wasanii na sekta ya Sanaa nchini kuendeshwa kwa weledi na kuongeza idadi ya vijana katika sanaa.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Abbdalah Ulega ameiagiza TaSUBa kutengeneza filamu ambazo zinaitangaza nchi yetu ikiwemo historia ya Nchi, Filamu ya Maisha ya Mwalimu Nyerere, Ushiriki wa Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika ili watanzania hasa watoto waijue historia ya nchi hii.
Halikadhalika, nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi ameongeza kuwa TaSUBa ni Taasisi kongwe ambayo iliundwa kimkakati katika kukuza Sanaa, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika Taasisi hiyo ili isaidie katika kuibua na kukuza vipaji vitakavyojiajiri na kutengeneza fursa kwa wengine.
Vilevile, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Herbet Makoye amesema katika mwaka huu wa masomo 2020/2021 chuo hicho kimeongeza udahili wa wanafunzi ambapo mpaka sasa kimedahili wananfunzi 651 lengo likiwa ni kuzalisha wataalamu wengi katika fani ya Sanaa.