Mbunge wa Jimbo la Madaba mkoani Ruvuma Joseph Mhagama akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lilondo jana kwa ajili ya kuwashukuru kutokana na kukipa kura nyingi chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba,pia alitumia mkutano huo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tano ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli
……………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Madaba
MBUNGE wa jimbo la Madaba Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma Joseph Mhagama,ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya na jitihada inazofanya za kuimarisha huduma za afya katika jimbo hilo.
Mhagama ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti, wakati wa mikutano yake ya kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba pamoja na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji na kata mbalimbali .
Amesema, kimsingi fedha hizo zinakwenda kuimarisha na kuboresha huduma za afya hasa ikizingatia kuwa katika jimbo hilo hakuna hospitali kubwa ya wilaya, badala yake wananchi wanategemea kupata matibabu katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo.
Amesema, wananchi wa Madaba hawana budi kumshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kazi kubwa aliyowafanyia ya kupeleka maendeleo na kusisitiza kuwa,heshima pekee wanayoweza kumpa Rais Magufuli ni kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi inayobuniwa na kutekelezwa na serikali ili kuleta tija.
Amesema mbali na fedha za ujenzi wa Hospitali ya wilaya, awali serikali ilishatoa shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Madaba na Mtyangimbole ambavyo vimeshakamilika na sasa wananchi wameanza kupata huduma za matibabu.
Pia amesema, serikali kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini Tarura imeanza ukarabati wa barabara ya Madaba kwenda Ifinga kata ya Matumbi yenye urefu wa km 48 ambayo wakati wa masika ilikuwa haipitiki kwa urahisi na hivyo wananchi kukosa huduma ya usafiri na kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Mhagama, amewataka wananchi wa jimbo la Madaba kuwa wazalendo na kuiga mfano wa Rais Dkt Magufuri ya kufanya kazi kwa kujituma ili kuondokana na hali ya umaskini, badala ya kuwa vibarua na kufanya kazi katika mashamba ya watu kutoka nje, jambo linaloweza kuchangia umaskini na hatari kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Aidha amewatahadharisha, kuepukana na tamaa ya fedha kwa kuuza ardhi yao kwa wageni ambapo amewahimiza vijana kutumia fursa ya ardhi iliyokuwepo kupanda miti na kulima mazao mbalimbali ya biashara na chakula ikiwemo zao maarufu la Parachichi ambalo lina soko kubwa hapa nchini.
Amesema, vijana kama nguvu kazi ya Taifa ni lazima watumie rasilimali ardhi kujikwamua na umaskini na kuacha tabia iliyozoeleka kulalamika na wengine kutumia muda wakazi vijiweni kucheza pool huku jukumu la uzalishaji mali wakiachiwa wazee, jambo linalopaswa kukemewa vikali.
“uchaguzi umekwisha, kwa hiyo ni lazima watu hasa vijana wajikite katika uzalishaji mali badala ya kuendelea kukaa vijiweni kupiga porojo zilizokuwepo wakati wa uchaguzi mkuu katika jimbo letu hatutaki kuona watu wakilalamika kwa kukosa ela kwani kuna fursa kubwa ya ardhi inayostawi mazao mbalimbali”alisema.
Mhagama ,amewataka vijana kutambua thamani ya maisha yao ni juu yao wenyewe na hakuna mtu anayeweza kutoka mbali kuja kuwasaidia fedha, bali juhudi zao ndizo zitakazo wainua kimaisha na kupata fedha kwa ajili ya kuhudumia familia zao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Theophanes Mlelwa alisema, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, kazi iliyobaki ni madiwani na watendaji wa serikali kuhakikisha wanashirikiana kutatua kero na changamoto za wananchi ili kuharakisha maendeleo.
Mlelwa ambaye ni diwani wa kata ya Wino, amewataka wananchi wa kata ya Wino na jimbo la Madaba kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa uchaguzi wa mwezi Oktoba na kuungana pamoja kuijenga Madaba yao ambayo inahitaji ushirikiano na umoja wa wananchi wote na sio kuiachia serikali.
Alisema, licha ya kuwa diwani wa kata hiyo, katika uongozi wake atahakikisha ana tenda haki kwa watu na kata zote na kuwataka wakazi wa kata ya Wino kutumia nguvu na maarifa kumaliza baadhi ya changamoto zilizokuwepo na pale watakapo shindwa basi halmashauri yao itaangalia namna ya kuwasaidia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea Nelly Duwe amesema, chama kina imani kubwa na Mbunge mteule Joseph Mhagama na diwani wa kata ya Wino Theophanes Mlelwa kutokana na uchapakazi wao,hivyo kuwataka kutobweteka na mafanikio baada ya kupita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu.
Amesema, hatua ya kupita bila kupingwa kwa viongozi hao wawili ni ishara kwamba wanakubalika kwa wananchi,kwa hiyo ili kudhihirisha hilo ni lazima wahakikishe wanashirikiana na wananchi wao kumaliza kero ambazo zinahitaji umoja wa pande zote mbili.
MWISHO.
Na Muhidin Amri,
Songea
WANANCHI wa kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya watumishi wa sekta ya Afya na dawa katika zahanati ya kijiji hicho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi na dawa.
Hayo yameelezwa jana na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliohudhuria mkutano wa kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi juu ya ufuatiliaji wa Uwajibikaji jamii uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali ROA kupitia mradi wa SAM unaofanya kazi katika sekta ya Afya kwenye kata tano za wilaya ya Songea.
Lucius Bula na Damian Mwenda wamesema, katika zahanati ya kijiji hicho kuna mganga mmoja na wauguzi watatu,hivyo kutokana na idadi kubwa ya watu inakuwa vigumu kwa watumishi hao kutoa huduma kwa wakati muafaka na kusababisha wagonjwa kutumia muda mwingi wakiwa foleni ya kuonana na Daktari.
Bula alisema,kwa sasa idadi ya watumishi waliopo ni ndogo kufuatia watu wengi hasa wageni wanaofika katika kijiji hicho na mikoa mingine hapa nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama kilimo na ufugaji ambao pindi wanapougua wanakimbilia zahanati ya Mgazini kupata huduma ya matibabu.
Kwa mujibu wa Bula,kuingia kwa wageni hao kumesababisha watumishi hao kuzidiwa na idadi ya wagonjwa na hivyo kusababisha baadhi ya wananchi kukimbilia Hospitali ya St Joseph Peramiho na wengine Hospitali ya mkoa Songea umbali wa km 45.
Damian Mwenda amesema, awali zahanati hiyo ilijengwa kuhudumia wananchi wa Mgazini tu, lakini sasa inalazimika kuhudumia wananchi wa vijiji vya jirani na ndiyo maana hata dawa zinazoletwa hazitoshelezi, kwa kuwa serikali inapeleka dawa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa kijiji kimoja na sio wa vijiji vingine.
Ameiomba serikali kupanua zahanati hiyo au kujenga kituo cha Afya ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi kwa wakati mmoja, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa ambao mara wanapofika ulazimika kutumia muda mwingi kuhudumiwa.
Kwa upande wake katibu wa mradi wa SAM James Simon amesema,mradi wa Sam unahusisha katika tano katika halmashauri ya wilaya ya Songea ambapo kazi inayofanya ni kufuatilia kama fedha zilizotolewa na serikali zimetumika vizuri katika Utekelezaji wa sekta ya Afya.
Amesema,lengo la mfumo huo ni kuwajengea wananchi uwezo wa kutafuta taarifa na kuzichambua ili waweze kufuatilia na kusimamia mipango,bajeti na Utekelezaji wa mkiradi mbalimbali katika maeneo yao.
James ameeleza kuwa,Sam inawezesha kuhoji uwajibikaji wa watendaji na watoa huduma, na kutolea mfano huduma za Afya ili hatimaye watumishi wa sekta hiyo waweze kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema, lengo la mfumo huo ni kuona watumishi na viongozi wote wa umma wanawajibika zaidi kwa wananchi wanaowatumikia na wananchi nao wanafahamu na kuelezwa wajibu wao kwa kufuatilia haki zao za msingi na kuwawajibisha watoa huduma wasiowajibika.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Songea Dkt Geofrey Kihaule amekiri kuwepo kwa tatizo la watumishi na dawa katika zahanati hiyo,hata hivyo amesema serikali imeandaa mpango mkubwa wa kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wanaofika katika zahanati ya Mgazini.
Amesema, zahanati ya Mgazini ni ya muda mrefu na ilijengwa kuhudumia wananchi wa vijiji viwili,kwa hiyo kutokana na wingi wa watu hasa jamii ya wafugaji waliohamia, kwa sasa changamoto iliyopo ni ufinyu wa eneo la kutolea huduma yaani majengo na dawa.
Hata hivyo amesema, kuna mpango kupitia benki ya Dunia wa upanuzi na ujenzi wa vituo ambapo zahanti ya Mgazini imebahatika kuwemo na imetengewa zaidi ya milioni 22 ambazo zitatumika kujenga jengo jipya ambalo litasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa.
Amesema, kwa sasa wanafanya mawasiliano na ofisi ya katibu tawala wa mkoa kutoa fedha hizo ili kuanza maandalizi ya ujenzi wa jengo la vyumba vitatu kwa ajili ya huduma ya Baba, mama na mtoto, na watu wanaoishi na VVU.
Amesema, wizara ya Afya na Tamisemi zimesisitiza kuwa ni muhimu kwa huduma za watu wanaoishi na VVU zitolewe katika jengo kubwa badala ya jengo la sasa ambalo ni dogo.
Alisema,kutokana na ongezeko kubwa la watu hasa jamii ya wafugaji kumekuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaokwenda kupata huduma katika zahanati hiyo,hata hivyo Halmashauri kupitia mapato ya ndani katika bajeti ya 2021/2022 imewek lengo la kukusanya mapato ya kutosha kwa ajili ya kununua vifaa tiba na dawa.
Amesema, mbali na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba mpango mwingine uliokuwepo ni kujenga zahanati mpya katika kijiji cha jirani ili kupunguza msongamano wa wananchi pindi wanapokwenda kupata huduma katika zahanati ya Mgazini.