Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Yinza akiongoza kikao cha Wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi wa Wanafunzi wanaotarajia kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2021 mkoani hapa jana.
Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu, akizungumza.
Na Godwin Myovela, Singida
WAJUMBE wa Kamati ya
Uchaguzi wa Wanafunzi wanaotarajia kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2021 mkoani
hapa wameazimia, pamoja na mambo mengine, kuanza mara moja ujenzi wa shule za
bweni walau moja kwa kila wilaya au halmashauri, lengo ni kupandisha kiwango
cha ufaulu.
Suala lingine
lililojitokeza katika kikao hicho ni kuwasihi wadau na wabunge wa maeneo husika
kujitokeza kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mchana kwa baadhi
ya shule hususani vijijini kutokana na wazazi kukosa uwezo sambamba na
jiografia ya maeneo husika kutokuwa rafiki.
Mjadala huo umefanyika leo,
wakati wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi kidato cha kwanza 2021 kilichofanyika
kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kwa kuhusisha Katibu Tawala na Afisa
Elimu Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa
Elimu ngazi mbalimbali na wadau wengine maalumu kutoka ndani ya halmashauri
zote 7 mkoani hapa.
Pamoja na hivi karibuni
serikali kuajiri walimu 314 lakini idadi hiyo imeonekana kuwa ni ndogo kuweza
kukidhi msawazo wa ikama uliopo baina ya walimu na wanafunzi, mathalani mpaka
sasa bado ni 1:78-150 hali inayozidisha wimbi la watoto wa shule za serikali
kutofanya vizuri sana, ikilinganishwa na zile za binafsi.
Aidha, kupitia mjadala huo,
baadhi ya maafisa utumishi waliombwa kujirekebisha na kuanza kuwajali, kuwa
karibu zaidi, kuwapenda na kusikiliza shida za walimu na sio kutoa lugha
chafu-ikiwemo kuwakatisha tamaa hasa pale wanapogubikwa na baadhi ya changamoto
za kimaisha, suala ambalo nalo limeelezwa kuchagiza ufaulu kuwa hafifu kwa baadhi
ya shule.
Huku baadhi ya wazazi nao
wakinyooshewa vidole kwa kukataza watoto kuhudhuria masomo kwa kigezo cha
kwenda kuchunga mifugo na shughuli nyingine, sanjari na kuwashawishi watoto
wasifanye vizuri pindi wanapoingia kwenye mitihani yao ya kitaifa, hali inayozidi
kuzorotesha kasi na juhudi za mkoa kufanya vizuri.
Afisa Elimu wa Mkoa wa
Singida, Nelasi Mulungu alikiambia kikao hicho kuwa kwa mwaka 2020 ufaulu katika Halmashauri 6 umeshuka
isipokuwa halmashauri ya Manispaa ndio pekee ambao wameongeza ufaulu kwa
asilimia 1.12, na kuitaka kila halmashauri
kujipanga na kuweka mikakati zaidi kwa ajili ya kuongeza ufaulu kwa mwaka 2021.
Mulungu
akizungumzia hali ya ufaulu ndani ya mkoa kwa mwaka 2020, alisema jumla ya wanafunzi 33,398 wakiwemo wavulana 15,727 na wasichana 17,671 walifanya mtihani wa kumaliza Elimu ya
Msingi. Kati ya wanafunzi hao waliofaulu
ni 23,785 wakiwemo wavulana 11,116 na wasichana 12,669. Ufaulu huo ni sawa na asilimia
71.89, huku waliofeli ni wanafunzi 9,613 sawa na asilimia 28.78.
“Ufaulu
wa mwaka huu 2020 ukilinganishwa na ule wa mwaka 2019 umeshuka kwa asilimia 3.13, aidha, idadi ya wanafunzi
waliofaulu imeongezeka kutoka wanafunzi 22,484 hadi 23,785,” alisema.
Akitoa tathmini ya matokeo hayo, Afisa Elimu huyo wa
mkoa, alisema ufaulu kwa baadhi ya masomo umepanda na mengine kushuka
ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2019. Mathalani, kwa somo la Kiswahili ufaulu
umepanda kwa asilimia 0.80, huku somo la Kiingereza likishuka kwa asilimia
9.25,
Alisema Maarifa ya Jamii limepanda kwa asilimia 3.66,
Hisabati limeshuka kwa asilimia 9.11, huku Sayansi nalo likishuka kwa asilimia
4.59.
Aidha,
akizungumzia kuhusu ugawaji wa nafasi za Kutwa, Mulungu alibainisha kuwa
ugawaji wa nafasi hizo umefanyika kufuatana na idadi ya wanafunzi waliofaulu
katika ‘Catchment’ yaani shule zinazozunguka sekondari fulani, ikilinganishwa
na idadi ya vyumba vya madarasa. Hata
hivyo, alisema jumla ya wanafunzi 23,726
wakiwemo Wavulana 14,423 na
Wasichana 12,192
wamepata nafasi katika shule za Kata.
Kuhusu
nafasi za Bweni, alisema Mkoa wa Singida umepatiwa nafasi 121 kwa aina ya bweni kawaida, bweni
ufundi na ufaulu mzuri, ambapo
nafasi za wavulana 78 na wasichana 43 kwa ajili ya wanafunzi hao
watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani
Kwa mujibu wa Ofisi ya Afisa Elimu Mkoa,
mpaka sasa jumla ya wanafunzi ambao hawajapata nafasi kwa chaguo la kwanza ni
524, na kati ya wanafunzi hao 488 wanatoka halmashauri ya Manyoni na Ikungi 36.
Pamoja na mambo mengine sababu hiyo imeelezwa kuchangiwa na upungufu wa
takribani vyumba 99 vya madarasa, ambavyo kwa agizo la serikali vinatakiwa viwe
vimekamilika kabla ya Februari 28, 2021.