******************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ya Rufiji,Mkuranga na Chalinze kuzifuatilia shule za msingi zilizofanya vibaya katika maeneo yao na kuhakikisha watapatia ufumbuzi changamoto zinazochangia kushuka kwake kitaaluma.
Aidha amezielekeza halmashauri, kumaliza kujenga miundombinu ya madarasa ifikapo january 28 mwakani 2021 ili kuhakikisha wanafunzi 7,850 watakaokosa nafasi madarasani awamu ya kwanza wanaweza kuendelea na masomo bila changamoto ya madarasa .
Akifungua kikao cha wadau wa elimu mkoani Pwani ,Ndikilo alisema haiwezekana kuona serikali inaongeza jitihada za kuboresha mazingira ya elimu huku tukishuhudia shule zinafanya vibaya bila kujua changamoto na kuzitatua .
Alieleza kati ya shule kumi zilizofanya vibaya kimkoa 2020 ,Ni pamoja na Kitapi kata ya Mbwara wilaya ya Rufiji wastani wa alama 81,Kibesa ya Mkuranga wastani 78.88 na Pera ya Chalinze yenye wastani 78.8.
Ndikilo amewaelekeza pia,wadhibiti wa ubora wa shule kwenda kukagua shule hizo ili ziweze kuimarishwa na kuinua hali ya kitaaluma .
Hata hivyo alipongeza mkoa huo kupanda ufaulu wa matokeo ya shule ya msingi kutoka asilimia 85.13 mwaka 2019 na kufikia asilimia 86.99 mwaka 2020 na kuwa nafasi ya 9 kitaifa .
“Tujitahidi tuweze kupanda pia kimkoa tutoke kundi la kumi bora na tufikie tano ama tatu bora ,walimu wapo na serikali inaendeleza elimu bila malipo hivyo hakuna sababu ya kushika mkoa” alifafanua Ndikilo.
Aliomba wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana na serikali kuchangia masuala ya kielimu ili kumaliza changamoto zilizopo za madawati na upungufu wa madarasa.
Pamoja na hilo ,kaimu katibu tawala wa mkoa huo Abdulrahman Mdimu ,alieleza licha ya kupanda ufaulu lakini lipo suala la mdondoko bado ni changamoto kubwa ambapo wanafunzi 157 hawakumaliza shule na hawajulikani walipo.