Kinamama na watoto wakisubiri huduma katika zahanati ya Kanoge.
Aliyeketi kushoto ni Dk. Omari Sukari mganga mkuu wa mkoa wa katavi akiwa na timu yake
****************************
Na Zillipa Joseph
Katavi
Ongezeko la watumishi wa idara ya afya mkoani Katavi limeelezwa kuleta mafanikio katika utoaji wa huduma mbalimbali hususan huduma za mama na mtoto
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa vijiji vya Ugalla, Kambuzi na Kabage katika Halmshauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamesema kwa sasa wakifika hospitali wanahudumiwa haraka na kuondoka
Bi. Maria Malendeka ni mkazi wa kijiji cha Kanoge anaeleza kuwa awali kinamama wenye watoto walilazimika kushinda siku nzima wakisubiri huduma katika zahanati ya Ugalla
“Ulikuwa unakuja hapa zahanati asubuhi ni mpaka jioni kabisa ndio unaondoka lakini sasa wahudumu wameongezeka ukikaa sana ni masaa mawili matatu” alisema Maria
Awali zahanati hiyo ilikuwa inahudumia vijiji vitatu Ugalla, Kambuzi na Kabage na ilikuwa na wahudumu watatu tofauti na sasa ambapo ina wahudumu watano
“Watoto walikuwa wanalia njaa kwa kukaa muda mrefu bila kula, unawadanganya na machungwa au muhogo lakini sasa ukiamua unakuja hapa au unakwenda Kanoge” aliongeza Maria
Bwana Pius Ndaji mkazi wa kijiji cha Kambuzi ameishukuru serikali kwa kujenga hospitali za wilaya na kuongeza watumishi
Bwana Apolinari Mushi ni Katibu wa Afya mkoa wa Katavi amesema wana ongezeko la watumishi 180 wa kada mbalimbali ambapo kwa mwaka 2018 walikuwa na watumishi 713 na sasa wana watumishi 893
Mushi amesema sanjari na ongezeko la watumishi wa idara ya afya pia kuna ongezeko la zahanati katika vijiji mbalimbali, vituo vya afya na hospitali
Ameongeza kuwa mwaka 2015 mkoa ulikuwa na jumla ya vituo vya afya 79 na hadi kufikia juni 2020 kuna vituo vya afya 101 ikiwa ni ongezeko la vituo 22
Aidha kuna Hospitali 1 ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali 3 za Halmashauri, na Zahanati 80 kati ya 65 zilikuzowepo
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dk. Omari Sukari amesema ongezeko hilo limeleta ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma za afya
Amesema kundi kubwa lililokuwa likiteseka lilikuwa ni la watoto wa kuanzia miaka sifuri hadi nane kwani ni kundi ambalo huwezi kulikosa wakati wowote unapofika katika sehemu za kutolea huduma za afya
“Hata vijiji ambavyo vimejenga zahanati vimesaidia kupunguza msongamano sehemu moja” alisema Dk. Sukari
“Hizi hospitali za wilaya nazo zimesaidia watu kuacha kuja mjini kutegemea hospitali moja kule wanapata huduma na maisha yanaendelea” aliongeza Dk. Sukari