Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah akizungumza katika kikao kazi cha washauri wa mifugo mikoa na wataalamu wa wizara katika kutekeleza mikakati ya sekta ya mifugo kuendana na llani ya Chama Tawala mkoani Singida leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbaraka Stambuli na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Deogratius Yinza.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Deogratius Yinza (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua kikao kazi hicho. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda, akizungumza katika kikao kazi hicho. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Stanford Ndibalema.
Afisa Mifugo Mkuu, Idara ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi, Mariam Mkachila akiwasilisha mada katika kikao hicho.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbaraka Stambuli akitoa mada katika kikao kazi hicho.
Afisa Mifugo Mkoa wa Pwani, Elisante Qadwe akiuliza swali katika kikao hicho.
Daktari wa Mifugo Mkoa wa Morogoro, Gasper Msimbe, akiuliza swali katika kikao hicho. Kushoto ni Daktari wa Mifugo kutoka Mkoa wa Mtwara, Subira Simbeye.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda, akiongoza kikao hicho, Kulia ni Afisa Utafiti wa Mifugo, Grace Masolwa.
Afisa Mifugo Mkoa wa Mara, Denis Ishengoma, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho,
Na Dotto Mwaibale, Singida
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imekuja na mipango saba yenye
lengo la kuboresha tija ya uzalishaji wa mifugo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah wakati akizungumza katika kikao kazi cha washauri
wa mifugo mikoa na wataalamu wa wizara katika kutekeleza mikakati ya sekta ya
mifugo kuendana na llani ya Chama Tawala mkoani Singida leo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2018/2019, wizara imeandaa na
kuanza kutekeleza mikakati saba ili kuendeleza sekta ya mifugo nchini. utekelezaji wa mikakati hiyo utaisadia Wizara kufikia dira na maono
iliyojiwekea tangu awali kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mifugo ya 2006.
Gillah alitaja malengo ya mikakati hiyo ni kuongeza
uzalishaji na tija, kudhibiti utoroshaji na biashara haramu za mifugo na mazao
yake, kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na mifugo na mazao yake ili Sekta
iweze kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa, kuepusha migogoro kati ya
wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, kulinda raslimali za mifugo zilizopo na
kuhifadhi mazingira.
Dkt. Gillah alitaja mikakati inayotekelezwa na wizara hiyo
kuwa ni kuboresha kosaafu za ng’ombe nchini, kudhibiti magonjwa na matumizi ya dawa, chanjo na viuatilifu vya wanyama nchini, kutafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji kwa mifugo, kuanzisha na kuwezesha ushirika wa wafugaji, kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake na kuboresha uzalishaji na biashara ya ndege wafugwao nchini.
Alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mikakati hiyo katika
maeneo mbalimbali nchini, wataalamu wa Wizara wanaosimamia utekelezaji wa
mikakati hii wamebaini uwepo wa elimu duni ya ufugaji bora na wa kibiashara kwa
wafugaji walio wengi, hususan wenye mifugo mingi na wanaohamahama na mifugo
yao.
Awali akifungua kikao kazi hicho Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa
wa Singida Deogratius Yinza alisema Sekta ya mifugo ni miongoni mwa Sekta za
kiuchumi ambayo ni muhimu katika kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa Taifa kwa
ujumla.
“Sekta hii inachangia katika kuwapatia wananchi ajira,
chakula, lishe, kipato na fedha za kigeni: Katika Mwaka 2019/2020 Sekta hii
imechangia asilimia 7.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 ya
mwaka 2018/2019 na kuwa Sekta hii imekua kwa asilimia 5 kwa mwaka 2019/2020
ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019 na kuwa hiyo imetokana na juhudi
zenu maafisa midugo, wafugaji na wadau wengine katika kufanya kazi kwa bidii
ili kuzalisha kwa tija.
Alisema nchi yetu ina rasilimali ya mifugo ambayo Wizara
inasimamia na kwa sasa inakadiriwa kufika ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni
21.29, kondoo milioni 5.65, kuku wa asili milioni 38.77, kuku wa kisasa milioni
44.51, nguruwe milioni 2.14 na punda wapatao 657,389.