Bi. Adelina Lyakurwa akijiu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na wananchi katika kijiji cha Ikola
Fundi kompyuta Rashid Othman akitengeneza kompyuta katika kijiji cha Isengule
******************************************
Kupatikana kwa huduma ya nishati ya umeme kwa wakazi wa vijiji vya Ikola, Karema na Isengule katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kumewezesha kufungua fursa kwa vijana kuanzisha biashara mbalimbali na kuwaondolea wakazi wa vijiji hivyo adha ya kuwa na vibaka
Wakizungumzia umeme huo unaotokana na mradi uunganishaji umeme vijijini REA III wananchi hao wamesema kwa sasa wanaishi kwa raha kama wako mjini
Pia wameeleza kuwa mwenendo wa shughuli mbalimbali umerahisishwa kama upatikanaji wa barafu kwa ajili ya kugandishia samaki, vinyozi wanaotumia mashine za umeme n.k
Flora Mwakasege ni mkazi wa kijiji cha Karema yeye ni fundi cherehani alisema kwa sasa anatumia mashine ya umeme hali inayomrahisishia kumaliza nguo za wateja wake kwa wakati
“Hapo mwanzo ilikuwa tabu hasa nyakati za sikukuu kama hizi ilikuwa tabu lakini sasa nashona hadi usiku na nikipita stendi yetu kote kweupe kunang’aa taa” alisema
Naye Musa Makali ni wa kijiji cha Isengule alisema ameweza kuanzisha biashara ya kurusha nyimbo katika simu za watu kwa kutumia kompyuta baada ya umeme kuwaka kijijini kwao
Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa njia za umeme Afisa Mahusiano na Wateja Tanesco mkoa wa Katavi Proches Joseph amewataka wananchi kutokulima mazao ya kudumu karibu na nguzo za umeme
Kwa upande wake Afisa Masoko kutoka TANESCO Makao Makuu Bi. Adelina Lyakurwa aliyefanya ziara ya uhamasishaji wananchi kujiunga na huduma ya nishati hiyo ya umeme wa REA III tatu amewataka wananchi kutumia wakandarasi wanaotambulika na TANESCO
“Ukitumia wakandarasi tunaowatambua ni rahisi kufuatilia linapotokea tatizo” alisema
Ameendelea kuwafafanulia wananchi kuwa gharama hizo za mkandarasi kutandaza nyaya katika nyumba zinabebwa na mteja ukiacha shilingi 27,000/- inayolipwa TANESCO kwa ajili ya uunganishaji huduma