Mshindi wa Haydom Marathon 2020 Herman Sulle (katikati) akikabidhiwa fedha na medali na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mbulu, Nicolaus Nsangazelu (kulia) na kushoto ni Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa Haydom Dkt Paschal Mdoe.
Washiriki wa mashindano ya Haydom Marathon wa chuo cha uuguzi Haydom HIHS wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumalizia mbio za kilomita 10.
Baadhi ya washiriki wa mashindano ya Haydom Marathon 2020, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay.
***************************************
Na Mwandishi wetu, Haydom
WANARIADHA 410 wa Mikoa ya Manyara, Singida na Arusha wamechuana vikali kwenye mashindano ya Haydom Marathon 2020 kwa lengo la kukusanya fedha za ujenzi wa wodi ya watoto wachanga ya hospitali ya rufaa Haydom.
Mkurugenzi wa tiba wa hospitali ya rufaa ya Haydom Dkt Paschal Mdoe akizungumza kwenye mashindano hayo amesema kwa mwaka huu wa 2020 lengo lilikuwa ni kukusanya shilingi milioni 100.
Amesema wamekusanya shilingi milioni 40 na wanaendelea kukusanya ili ifike lengo la kukusanya shilingi milioni 100 ambazo watazichanganya na zile shilingi milioni 100 za mwaka jana ili ujenzi wa jengo jipya la wodi ya watoto wachanga uanze mapema Januari 2021.
Amesema lengo lao ni kufikisha shilingi milioni 300 ili kufanikisha gharama za ujenzi hivyo kupitia mashindano hayo na michango ya wadau wengine watafanikisha fedha za ujenzi wa jengo hilo la watoto wa changa.
“Kwenye wodi ya watoto hivi sasa wa siku ni kati ya 20 hadi 30 awali tulikuwa na watoto watano au sita, jengo la sasa ni dogo, linahitajika lingine ambalo litawekewa vifaa vingi zaidi vya teknolojia,” amesema Dkt Mdoe.
Amesema mbio hizo zinatarajiwa kuendelea tena mwezi Mei mwaka 2021 kwa lengo la kuchangia wodi hiyo ya watoto wachanga kupitia Haydom Marathon Run for life saves neonates.
Katika mashindano ya mbio za kilomita 21 mwanariadha chipukizi kutoka kata ya Endamilay wilayani Mbulu, Herman Sulle alishika nafasi ya kwanza na kujipatia shilingi 250,000 kwa muda wa 1.06.13.95 Joseph Martin wa wilaya ya Babati alishika nafasi ya pili kwa muda wa 1.06.35.31 na kujipatia shilingi 125,000 huku Anthony Moya wa wilaya ya Hanang’ akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 1.06.48.85 na kujipatia shilingi 75,000.
Kwa upande wa wanawake kilomita 21 mshindi alikuwa Tunu Andrea wa mkoani Singida aliyejtumia muda wa 1.28.16.75 nakujipatia shilingi 250,000 huku mshindi wa pili Neema Sanka wa Karatu akijipatia shilingi 125,000 na kutumia muda wa 1.32.52.71 na watatu ni daktari wa hospitali ya rufaa ya Haydom, Dkta Laura Chuwa aliyepata shilingi 75,000 kwa kutumia muda wa 1.59.90.91.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga akizindua mashindano ya Haydom Marathon kilomita 21, kilomita 10 na kilomita mbili alisema Mbulu ndiyo chimbuko la riadha nchini.
Kamoga amesema huwezi kuzungumzia historia ya riadha nchini bila kumtaja mwanariadha maarufu Stephen John Akwary ambaye ametokea wilayani Mbulu.
Amesema eneo la Mbulu ni sahihi kwa serikali kuweka kambi kuliko kuweka maeneo yenye kiwango cha juu cha joto kwani Haydom hali ya hewa kutoka usawa wa bahari ni nzuri na inafaa kwa riadha.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay amesema michezo ni afya kwani ukishiriki utakuwa mbali na daktari hasa kwenye magonjwa yasiyoambukizwa ya kisukari na shinikizo la damu.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu, Nicolaus Nsangazelu amewapongeza washiriki wote na waandaji wa Haydom Marathon.
Mwanafunzi wa utabibu wa chuo cha uuguzi Haydom (HIHS), Glory Naman amesema ameshiriki mbio hizo siyo kea lengo la mashindano bali kuchangia wodi ya watoto wachanga.
Mwanafunzi mwingine wa utabibu wa chuo cha uuguzi Haydom (HIHS), Sweetbert Msofe amesema jamii inapaswa kuunga mkono mbio hizo kwa kushiriki riadha endapo zitafanyika tena mwezi Mei 2021.