***********************************
Uamuzi huo umetolewa na Jaji A.Z Mgeyekwa baada ya kubaini wakati anatoa uamuzi wa kutengua hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Bodi ya Msikiti wa Ijumaa haikuwa uwakilishi mahakamani hapo.
Akitoa uamuzi mdogo kwenye kesi ya maombi ya mapitio (riview) namba 2/2020 yaliyotokana na rufaa namna 30/2020 iliyofunguliwa na Bodi ya Thaqaafa dhidi ya Bodi ya Msikiti wa Ijumaa,Jaji Mgeyekwa alisema,ameangalia mambo mengi na kubaini msikiti wa Ijumaa haukuwa na uwakilishi kwenye kesi hiyo.
Alisema Bodi ya Thaqaafa ilifungua kesi kwenye Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana dhidi ya Bodi ya Msikiti wa Ijumaa ambayo iliamua kuwa Bodi ya Thaqaafa iheshimu mkataba wa upangaji baada ya kusaini mkataba na msikiti.
“Mkataba uliokuwa ukibishaniwa mahakamani, Idrisa Haeshi alisaini kama mdhamini wa Bodi ya Thaqaafa,ajabu huyo huyo aliyesaini kama mdhamini kuwa mlalamikaji na mdaiwa (mjibu rufaa) wa Bodi ya Msikiti,”alisema Jaji Mgeyekwa na kuongeza;
“Kwa mgongano huo haiwezi kuthibitika kulikuwa na uwakilishi halali wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa kwenye shauri la rufaa namba 30/2020, kwa msingi huo nafuta uamuzi wa awali,sasa uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana utabaki ulivyo.”
Jaji Mgeyekwa alisema Bodi ya Thaqaafa ikijisikia kuendelea na rufaa yao wapeleke hati ya wito mahakamani kwa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa ili rufaa hiyo iendelee kukiwa na uwakilishi wa pande zote.
Wakingumza nje ya mahakama, Mjumbe wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa, Sherally Hussein Sherally na Katibu wa Bodi ya Msikiti huo, Abdallah Amin Abdallah, walisema mahakama imetenda haki.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu na Jaji kwa maamuzi aliyotoa ya kufuta uamuzi wa awali baada ya kuona msikiti haukuwa na uwakilishi kwenye rufaa ya Thaqaafa.Huu ni ushindi ssa tutachukua hatua stahiki baada ya kushauriana na mawakili wetu,”alisema.
Naye Katibu wa Bodi hiyo, Abdallah alisema mahakama imetenda haki na hana zaidi ya kumshukuru Mungu kutokana na dhuluma iliyotaka kufanyika dhidi ya msikiti na kwa hali hiyo Thaqaafa lazima walipe deni la pango sh. milioni 58 wanazodaiwa na msikiti na kwa miaka minne sasa limeongezeka.
Bodi ya Thaqaafa ilifungua kesi namba 11/2019 kwenye Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana ikipinga kulipa kodi ya pango sh. milioni 58 kwa mujibu wa mkataba wa upangaji kwenye Zahanati ya Msikiti wa Ijumaa Machi, 2015, wakidai licha ya kuwa ni wapangaji hawastahili kulipa.
Mahakama hiyo chini ya Hakimu Gwaye Sumaye alitoa uamuzi ikiitaka bodi hiyo kuheshimu mkataba huo wa upangaji wa 2015 ambapo Bodi ya Msikiti ilikaza baada kushinda kesi.
Hata hivyo, Bodi ya Thaqaafa haikuridhika na hukumu hiyo ambapo Mei 30,2020 ilikata rufaa namba 30 ya 2020 kwenye Mahakama Kuu Mwanza,shauri ambalo liliendeshwa hadi Septemba 16,2020 na kutolewa hukumu dhidi ya Bodi ya Msikiti wa Ijumaa.
Aidha Bodi ya Msikiti wa Ijumaa baada ya hukumu hiyo ilifungua maombi ya Marejeo (Riview) namba 2/2020 mahakamani hapo wakidai hawakuwahi kupata wito wa kufika mahamakani kujibu rufaa iliyoipa ushindi Bodi ya Thaqaafa,hukumu iliyotolewa leo/jana.sss