Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) Dkt. Bedan Masuruli akizungumza na mifugouvuvi Online Tv juu ya wataalamu 19 wa afya ya wanyama ambao wameshindwa kuwasilisha taarifa za magonjwa ya mifugo katika halmashauri za wilaya wanazotoka kwa Udara ya Huduma za Mifugo iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
**************************************
Na. Edward Kondela
Wataalamu tisa wa afya ya wanyama kutoka halmashauri za wilaya hapa nchini, wamepewa onyo kali kwa kutowasilisha taarifa za magonjwa ya mifugo kwa Idara ya Huduma za Mifugo iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi huku wataalamu 10 wakipewa wiki moja kuwasilisha ushahidi wa wao kuwasilisha taarifa hizo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki (12.12.2020) na mifugouvuvi Online Tv inayomilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kando ya kikao cha 38 cha Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania (TVA) kilichofanyika Mkoani Arusha kuanzia Tarehe 10 hadi 12 Mwezi Desemba Mwaka 2020, Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) Dkt. Bedan Masuruli amesema wataalamu tisa wametakiwa katika kipindi cha mwaka mmoja hawakosi kabisa kutoa taarifa kwa idara hiyo kila wiki na kila mwezi.
Dkt. Masuruli amefafanua kuwa Tarehe 9 Mwezi Desemba Mwaka 2020, baraza liliitisha kikao cha dharula kujadili maadali kwa wataalamu mbalimbali ambao wamekuwa wakishindwa kutoa taarifa za magonjwa kwa Idara ya Huduma za Mifugo, ambazo zinatakiwa kila wiki na kila mwezi ambapo takriban asilimia 40 za wataalamu hawatoi taarifa hizo kati ya wilaya 184.
Ameongeza kuwa wataalam 78 walikuwa hawatoi taarifa, hata hivyo baada ya kufanya mahojiano ya awali wataalamu 34 walibakia kutotoa kabisa taarifa na baraza katika kikao hicho limewaita wataalamu hao kutoka halmashauri mbalimbali za wilaya, ambapo 19 wameitikia wito na wamefika katika kikao maalum cha baraza.
Aidha, amesema katika mahojiano wataalamu 10 ambao wamesema wanaoushahidi wamepewa wiki moja ili kuwasilisha ushahidi huo kabla ya uamuzi kufanyika lakini wataalamu tisa ambao walionekana hawana ushahidi wamepewa onyo kali na kuhakikisha katika kipindi cha mwaka mmoja hawakosi kabisa kutoa taarifa za magonjwa kwa Idara ya Huduma za Mifugo kila wiki na kila mwezi.
Pia, Msajili huyo wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) Dkt. Bedan Masuruli amesema baraza kwa kushirikiana na Idara ya Huduma za Mifugo litaendelea kutoa elimu kwa wataalamu wa afya ya wanyama juu ya umuhimu wa taarifa za magonjwa ya mifugo kutoka katika halmashauri za wilaya wanazofanyia kazi ili wafahamu umuhimu wa taarifa hizo katika kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
Idara ya Huduma za Mifugo iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikipokea taarifa za magonjwa ya mifugo kila wiki na kila mwezi ili kufahamu mwenendo wa hali ya magonjwa katika maeneo mbalimbali nchini na namna ya kukabiliana nayo pamoja na kupanga mpango wa kuzuia na kutokomeza magonjwa ya wanyama.