Mkuu wa chuo Cha maendeleo ya jamii Monduli, Elibariki Ulomi akizungumza katika mahafali ya 11 ya chuo Cha mendeleo ya jamii Monduli ambapo jumla ya wahitimu 779 walihitimu masomo yao ngazi ya stashahada na astashahada.(Happy Lazaro)

Baadhi ya wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja katika mahafali ya 11 ya wanafunzi wa chuo Cha maendeleo ya jamii Monduli ambapo jumla ya wanafunzi 779 walihitimu kozi mbalimbali (Happy Lazaro)
*****************************************
Happy Lazaro,Arusha.

Katibu mkuu wizara ya afya , maendeleo ya jamii jinsia Wazee na Watoto ,Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii,Dkt. John Jingu amewataka wahitimu wa taaluma ya maendeleo ya jamii kubuni mbinu mbalimbali za kuweza kujiajiri badala ya kuchagua kazi ili waweze kuleta mbadiliko chanja katika jamii.

Aliyasema hayo leo wakati akizungumza katika mahafali ya 11 ya wahitimu  wapatao 779 katika ngazi ya stashahada na astashahada katika  chuo cha maendeleo ya jamii Monduli.
Dkt. Jingu ,aliwataka wahitimu hao kufikiria nje ya boksi na kujiajiri katika shughuli mbalimbali , badala ya kusubiria kupata kazi waliyosomea badala yake wajiongeze na kutochagua kazi .
Aidha aliwaasa kuleta matokeo chanja katika jamii inayowazunguka kupitia elimu waliyoipata kwa kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuweza kuleta ufumbuzi.
“Naombeni sana ndo mmehitimu kozi zenu Sasa hivi msiende kukaa tu mkisubiria kuajiriwa katika fani ya maendeleo ya jamii ,badala yake mjiongeze kwa kujiajiri huku mkileta matokeo chanja katika jamii na kuleta majawabu ya changamoto kwa jamii kwa kile mlichosomea.”alisema Dkt. Jingu.
Naye Mkuu wa chuo hicho,Elibariki Ulomi alisema kuwa chuo hicho ambacho kimeanzishwa mwaka 1977 kimekuwa kikitoa elimu katika fani hiyo ambapo kimetoa wanavyuo wengi ambao wameweza kujiajiri na hata kuajiriwa katika ngazi mbalimbali.
Ulomi alisema kuwa,pamoja na kuwepo kwa mafanikio mbalimbali wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya miundombinu ambapo wana uhitaji wa vyumba vya mihadhara vitatu,mabweni 3 pamoja na watumishi katika nyanja mbalimbali wapatao 11.
Hivyo waliomba kuboreshewa miundombinu chuoni hapo ili kuweza kupata wanafunzi wengi zaidi kulingana na uhitaji uliopo.
Naye Mbunge wa Monduli,Fredy Lowassa alisema kuwa ,chuo hicho kimekuwa msaada mkubwa sana kwa jamii ya wananchi wa Monduli  na mikoa mingine kutokana na elimu inayotolewa kuwa bora na yenye kutoa wataalamu waliobobea zaidi.
Fredy aliwaasa wahitimu hao kutumia mitandao ya kijamii vizuri kwa kuelimisha jamii badala ya kuitumia viabaya ambayo mwisho wa siku huchangia kupotosha jamii endapo itatumika tofauti.
Akisoma risala ya wahitimu,Mmoja wa wahitimu  Alhaji Abdala alisema kuwa,uongozi mpya uliopo chuoni hapo hivi Sasa wameweza kukibadilisha chuo hicho kwa kutoa elimu shirikishi ambayo itawawezesha wao kuweza kujiajiri na hata kuweza kuajiri wengine.
Aidha alisema kuwa,kwa sasa hivi nafasi ya ajira ni chache sana hivyo wanashukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kuweza kujiajiri ,hivyo aliomba vyuo mbalimbali kuongeza wigo wa kuweza kuwaunganisha wahitimu na fursa mbalimbali za ajira.