…………………………………………………………………….
Mbunge wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma, Deo Ndejembi ameafanya ziara ya kukagua miundombinu ya barabara jimboni kwake pamoja na kuzungumza na wakulima wa zao la miwa ambao amewaahidi kuwaletea wafadhili watakaowekeza zaidi ya Sh Bilioni Mbili kwenye kilimo hicho.
Ndejembi ametoa ahadi hiyo alipokua akizungumza na wakulima wa zao la miwa wa kata ya Dabalo ambapo alifanya nao kikao kifupi cha kujadili na kutambua changamoto wanazozikabili Ikiwa ni ziara yake ya kwanza jimboni tangu achaguliwe kwa kishindo kuwa Mbunge wa Chamwino.
Amesema ziara yake hiyo ya kwanza imehusisha wataalamu kutoka Tarura ambapo amepita nao kwenye kila barabara yenye changamoto na kukubaliana nao kuanza kufanya maboresho na ujenzi wa miundombinu hiyo ili wananchi hao wasipate tabu ilihali jimbo lao ni Jimbo ambalo hadi Rais Dk John Magufuli anaishi kwa maana ya Ikulu.
” Ndugu zangu nimekuja pamoja na kuwashukuru kwa kunichagua mimi na Rais Magufuli lakini nimekuja kuangalia hali ya miundombinu nikiambatana na wataalamu wetu wa Tarura ili kwenye yale maeneo korofi ambayo yameathiriwa pengine na mvua basi ujenzi uanze mara moja kuhakikisha barabara na vivuko vyote vinakaa sawa.
Ndugu zangu wakulima wa miwa niwaahidi kushirikiana nanyi kwenye zao hili ambalo linastawi sana kwenye ukanda wetu huu, tujiekee utaratibu wa ushirika, kilimo cha pamoja tukuze tija yetu ya mavuno ya miwa na wawekezaji watakuja tu, lakini tayari nimezungumza na mojawapo ya Benki kubwa nchini wamekubali kuwekeza zaidi ya Bilioni mbili hapa kwetu Dabalo, kwahiyo tusikubali kuachia hiyo fursa.
Nisingeweza kuja nao leo bila mimi mwenyewe kuja na kuwaona nyie wahusika, sijui mmejipanga vipi na mikakati yenu ya kuongeza tija, lakini niwahakikishie hizo Bilioni mbili ndani ya muda mchache hawa wenzetu wa Benki wataleta hiyo fedha lakini muhimu ni sisi kukaa na kuweka ushirika wetu katika namna ya kisasa zaidi,” Amesema Ndejembi.
” Niwaombe muweke sawa katiba yenu na uongozi wenu kwa sababu lengo kubwa ni kuhakikisha tunawanyanyua kiuchumi, tunalima miwa ili kupata kipato na ndio lengo kubwa la Rais wetu Magufuli, sisi kilimo ndio dhahabu yetu lakini ni lazima tufanye kilimo chenye tija kitakachokuza uchumi wetu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” Amesema Ndejembi.
Amesema mara baada ya ziara hiyo ya kukagua miundombinu ya barabara atafanya ziara ya kukagua sekta ya elimu, maji na afya na baada ya hapo utekelezaji wa ilani ya CCM ndio utakaofuata ili kukamilisha yale yote yaliyopo kwenye ilani hiyo.