Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kutoka kwa uongozi wa kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha, namna kiwanda hicho kinavyotumia mitambo mbalimbali kutengeneza bidhaa zitokanazo na maziwa.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua moja ya mitambo iliyopo katika kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha, alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kiwanda hicho ili kujionea ubora wa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akinyanyua moja ya vibebeo maalum vinavyotumika kukusanyia maziwa kutoka kwa wafugaji, wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kiwanda cha maziwa Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akipata maelezo ya moja ya bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Irfhan Virjee.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akifunga kasha la kubebea maziwa kwa kutumia mashine maalum wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha.
********************************************
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema uzalishaji wa maziwa nchini unazidi kuongezeka kutoka lita bilioni 2.7 kwa mwaka hadi lita bilioni 3.01, huku matumizi ya maziwa yakiripotiwa kuwa bado yako chini.
Akizungumza jana (02.12.2020) alipotembelea kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited kilichopo Mkoani Arusha ili kujionea namna viwanda vya maziwa vinavyozingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha, Prof. Gabriel amesema bado jitihada zinatakuwa katika kuhamasisha wananchi kunywa maziwa katika kuboresha afya zao.
“Matumizi ya maziwa nchini ni lita milioni nane kwa siku, ambapo kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kila mtu anatakiwa kunywa lita 200 kwa mwaka lakini kwa Tanzania unywaji wa maziwa kwa mtu umefikia walau lita 54 kwa mwaka, natoa wito kwa watanzania waongeze bidii katika matumizi ya maziwa kwa ajili ya kuboresha afya zao kwa maana ya akili na uimara wa mwili.” Amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel ametoa wito kwa sekta binafsi hususan waliopo kwenye tasnia ya maziwa nchini, kuendelea kuiunga mkono serikali kwa kuhakikisha wanaongeza thamani ya bidhaa zao pamoja na kuziweka kwenye vifungashio tofauti kulingana na mahitaji ya wateja wao.
Aidha, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inahakikisha inaboresha kosaafu na mbari ya mifugo kwa kutumia njia ya uhimilishaji ili azaliwe ng’ombe mwenye ubora, pia kuzingatia afya ya mifugo kwa kutoa chanjo na mifugo kuogeshwa pamoja na uwepo wa malisho bora.
Pia, ametoa wito kwa wenye viwanda vya maziwa nchini kuhakikisha wanafikia uwezo wa kiwanda uliosimikwa katika uzalishaji wa maziwa kwa kuwa ni hasara kuzalisha kidogo tofauti na uwezo wa kiwanda kwani kwa kufanya hivyo wenye viwanda wanapata hasara na pia serikali inapata mapato kidogo kutokana na tozo mbalimbali.
Amewakumbusha pia wenye viwanda vya maziwa kuzalisha bidhaa bora ili watanzania wawe na imani na viwanda vyao na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo ajira zitaongezeka pamoja na mapato ya serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Galaxy Food and Beverages Limited Bw. Irfhan Virjee amemwambia katibu mkuu huyo kuwa Tanzania inatakiwa iwe nchi ya pili kwa kuzalisha maziwa mengi na kusambaza katika nchi mbalimbali, kwa kuwa ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na mifugo mingi na kwamba soko la maziwa bado ni kubwa.
Bw. Virjee ameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuwa kiwanda hicho kimeanzishwa katika serikali ya awamu ya tano na kubainisha kuwa uzalishaji utazidi kuongezeka kutokana na uwepo wa masoko kutoka ndani na nje ya nchi.