MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati ametoa wiki mbili kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuhakikisha wamerudisha maji katika Soko Kuu.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kukagua masoko ya Tabora kwa ajili ya kujionea matatizo mbalimbali wanayokabiliana nayo wafanyabiashara.
Dkt. Sengati alichukua hatua hiyo baada ya kutembelea soko kuu wa kukuta maji yamekatwa na wafanyabiashara wa soko hilo wakiendesha shughuli zao bila ya kuwa na maji ya uhakika.
“Nataka hapa watu wapate maji ya uhakika ndani ya wiki mbili …angalie katika ‘strategic area’ muweke maeneo ya watu kupata maji ambayo yatawasaidia kufanya biashara zake bila matatizo” alisema.
Dkt. Sengati alisema utatuzi wa tatizo la maji katika soko hilo na mengine lazima ufanyike haraka ili kulinda afya za wafanyabiashara hao.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Tabora kukutana na viongozi wa Masoko ili kuweka mpango wa endelevu wa kuhakikisha maji hayakatwi na Mamlaka ya Maji kwa sababu ya watumiaji kushindwa kulipia bili.
Katika hatua nyingine Dkt. Sengati ameuagiza Uongozi wa Manispa ya Tabora kuhakikisha wanaweka umeme na kuziba nyufa katika paa katika Soko kuu na soko la Kachoma kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa bidhaa za wafanyabiashara hao katika masoko hayo.
Alisema uongozi wa Manispaa utakaliwa mpango wa muda mfupi wa kuhakikisha unaondoa mapungufu yaliyojitokeza katika soko la Kuu na soko la Kachoma kwa ajili ya kuwawekea mazingira mzuri ya wafanyabishara hao kufanya biashara zao katika mazingira rafiki.