****************************************
Na John Walter-Babati
Mbunge wa jimbo la Babati mjini Pauline Gekul (CCM) amewapongeza Tarura kwa hatua walizochukua kuwarudishia mawasiliano wananchi kwa kuwa walikuwa wanalazimika kutumbukia kwenye mtaro na kuvutana ili kufika upande wa pili.
Mbunge huyo ameyasema hayo akiwa mtaa wa Miyomboni wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti akikagua miondombinu ya eneo hilo ambalo lilikosa mawasiliano kwa muda mrefu baada ya kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana.
“Mimi napendaga kusema ukweli, hapa tulikuwa tunavusha watoto na kimsingi bajeti hii niliongea na Meneja wa Tarura Mjini Babati tukaomba tusaidiwe” alisema Gekul
Ameongeza kuwa maombi ya kurekebishwa kwa bara bara ya Miyomboni alipeleka kama matano kwa Wizara na kwa katibu mkuu wa TAMISEMI ambapo alijibiwa kuwa, kwa kuwa wamepewa bara bara ya Chemchem hivyo wavute subira wakati wanashugulikia hayo mengine.
Katika hatua nyingine Gekul amewaomba TARURA waweze kuimarisha daraja hilo la Miyomboni ili magari yaweze kupita kusambaza nguzo za TANESCO na hatimaye wananchi wapate huduma ya Umeme.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TARURA) halmashauri ya mji wa Babati Innocent Mungi ameeleza kuwa Bara bara ya miomboni ina urefu wa Kilomita 3.28 ambapo inaunganisha bara bara inayoelekea Singida na kuishia kijiji cha Nakwa.
Amesema kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwaka 2019 bara bara hiyo ilikatika baadhi ya maeneo ambapo ofisi ya TARURA Mjini Babati ilifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata mawasiliano na kuendelea kupata huduma zote muhimu kwa kuweka Kalavati la chuma ambalo walilitoa kutoka daraja la Mruki.
Amesema kwa sasa wanasubiri bajeti ya mwaka 2020-2022 ili kuweka box kalavati.
Meneja wa Wakala wa Barabara mjini na vijijini (TARURA) mkoa wa Manyara Mhandisi Slaa, amesema wakati TARURA inaanzishwa mwaka 2017 haikuwa kwenye mtandao wa barabara za ujenzi Babati Mji hivyo haikuwekwa kwenye bajeti iliyopita ya kwa kuwa ni mpya na kwa sasa watakachokifanya ni kupunguza bajeti iliyotengwa kwa ajili ya bara bara zingine na kuhamishia kwenye zingine ambazo hazikupangiwa.