*****************************************
Na Mwandishi Wetu
KANISA Karmeli Deliverance Ministry International la Tangi bovu, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam, linatarajia kufanya sherehe kubwa itakayoambatana na chakula cha usiku (Dinner party) Desemba 06, mwaka huu, ikiwa ni njia moja wapo ya kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha kufikisha miaka tisa ya huduma.
Akizungumza kanisani hapo hivi karibuni, mbeba maono wa Karmeli, Mchungaji na Nabii Dk Enock Mwasambogo alisema, licha ya kupitia mambo mepesi na mazito, vikwazo na changamoto mbalimbali katika kuendesha huduma ya Mungu, imekuwa ni neema kwake na kwa wana jamii ya Karmeli kufikisha miaka hiyo tisa ya kulitangaza neno la Mungu na kutoa huduma nyingine za kiroho, ikiwemo kufungua waliofungwa na nguvu za giza.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo Mkuu wa Karmeli-Mlima wa Majibu, si kwa nguvu wala akili za mwanadamu mambo mengi mema yamewezekana katika kanisa hilo, bali ni kwa msaada wa Mungu.
Kutokana na hilo, alisema “Kila mwana Karmeli pamoja na wote wanaoitakia mema huduma ya Mungu katika Karmeli, hawana budi kufurahia kwa pamoja kanisani hapo kwa chakula cha usiku, siku hiyo ya Desemba 06.
Usiku huo uliopewa jina Dinner Party, utapendezeshwa na burudani za aina mbalimbali, ukiwemo uimbaji wa nyimbo zinazompa Mungu Sifa na Utukufu kutoka kwa waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka ndani na nje ya kanisa hilo.
“Shetani huwa hapendi kuona watu wa Mungu wanafumguliwa kutoka katika minyororo aliyowafunga ndio maana amekuwa akichochea vita kila wakati kuhakikisha makanisa ya Mungu hayasongi mbele…kutokana na ukweli huo, ikiwa Karmeli tumeweza kumshinda kwa kishindo na kuifikia miaka tisa ya huduma, basi tunayo kila sababu ya kusherehekea,”alisema.
Dk Enock alieleza zaidi kuhusu sherehe hiyo na kusema kuwa itaanza kwa ibada maalumu asubuhi ya saa 12:30 hadi saa 3:30 asubuhi, ambapo washirika watakwenda nyumbani na kurejea jioni ya saa 11:00 kwa ajili ya chakula cha usiku kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine watakuwa wamekidhi vigezo na masharti ya kuhudhuria sherehe hiyo.
Alisema katika ibada ya asubuhi washarika watatakiwa kuvaa mavazi meupe kuashiria utakatifu na wakati wa usiku watavaa nguo za aina yoyote ilimradi ziwe za heshima, kwaajili ya utukufu wa Mungu.
Kwa maelezo ya Nabii Dk Enock, Sherehe hiyo itahudhuriwa na waalikwa mbalimbali, wakiwemo manabii, mitume, wachungaji, waalimu wa neno la Mungu, wainjilisti (waimbaji wa injili) pamoja na wapendwa wengine, bila kubagua dini wala madhehebu yao.