Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wakimkaribisha mgeni rasmi (hayupo kwenye picha), wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akisisitiza jambo mbele ya Waganga Wakuu wa Mkoa na Waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.HAKIKISHENI UKOMA UNATOKOMEA NCHINI TANZANIA.
Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote akieleza jambo wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.
Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini Dkt. Zuweina Kondo Sushy akifuatilia neno kutoka kwa Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.
*************************************
Na Rayson Mwaisemba WAMJW- DOM
Mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa mikoa wote kutumia mbinu mbali mbali ili kuutokomeza ugonjwa wa ukoma na Kifua Kikuu nchini Tanzania.
Dkt. Subi ametoa wito huo leo wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa Mpango wa taifa wa kudhibiti kifua Kikuu na ukoma uliohudhuriwa na Waganga wakuu na Waratibu wa kifua Kikuu na ukoma ngazi ya Mkoa, uliofanyika Jijini Dodoma.
“Tumieni kila liwezekanalo ugonjwa wa ukoma uishe nchini Tanzania, kwa Waganga Wakuu wa Mkoa ambao Halmashauri zenu bado zina maambukizi ya ukoma jipeni ndani ya miaka mitano ugonjwa wa ukoma utoweke nchini ” amesema Dkt. Subi.
Dkt. Subi amesema kuwa, ni muhimu kwa viongozi kutumia takwimu ili kuwasaidia katika kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati katika utekelezaji wa majukumu yao, jambo litalosaidia kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini.
Aidha, Dkt. Subi ametoa agizo kwa Waganga Wakuu wa mikoa wote kuhakikisha maelekezo na maazimio yaliyotokana na Mkutano huo yatolewe kwa maandishi kwa Halmashauri zote nchini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kutokomeza ugonjwa wa Ukoma na Kifua Kikuu.
Mbali na hayo, Dkt. Subi ameagiza kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa umma kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kama vile radio za jamii, mitandao ya jamii, ili kuwakinga wananchi wetu dhidi ya maambukizi ya magonjwa ikiwemo ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma.
“Toeni elimu ya Afya kwa wananchi, wananchi waelimishwe kuhusu magonjwa mbali mbali katika Jamii ikiwemo ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma, wekeni utaratibu wa vipindi vya Afya kwenye radio za mikoa yenu” amesema Dkt. Subi.
Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote amemhakikishia Mgeni rasmi kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na ukoma nchini.
“Sisi kama Ofisi ya Rais TAMISEMI tumejipanga kusimamia utekelezaji wa maazimio yote ambayo yametokana na Mkutano huo ili kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini “amesema Dkt. Çhawote.